Samia asema historia chachu kukuza utalii

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 01:20 PM Apr 25 2024
RAIS Samia Suluhu Hassan.
PICHA: MAKTABA
RAIS Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuna haja ya kutumia historia mbalimbali zilizopo nchini ili kukuza utalii na kuongeza pato la taifa kama ambavyo mataifa mengine yanafanya duniani.

Rais Samia amesema hayo Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwenye hafla ya utoaji wa nishani za Muungano pamoja na uzinduzi wa vitabu vya Historia ya Muungano na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Amesema kama historia zilizopo nchini zitawekwa vizuri, zitasaidia kukuza utalii kama ambavyo mataifa mengine yamekuwa yakifanya na kuyaingizia mapato na hatimaye kukuza uchumi.

"Wenzetu wanatumia historia za mataifa yao kukuza utalii. Watu  wanatoka katika mataifa mengine kwenda kujifunza historia ya taifa lingine, hivyo basi kama historia ya taifa letu, ikiwamo hii miaka 60 ya Muungano tutaitumia vizuri, tutakuza utalii.

"Nilikuwa Uturuki hivi karibuni, wenzetu wanatumia historia ya taifa lao watu kwenda  kutalii kujifunza namna ambavyo walipigana vita wakapata eneo lakini pia baadaye wakapokonywa," amesema.

Pia amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, mshikamano na uzalendo kuulinda Muungano ambao mwaka huu unatimiza miaka 60.

"Pia nitoe wito kwa Watanzania kusoma vitabu hivi ili kuenzi kazi nzuri iliyofanywa.  Lakini  kusoma vitatu hivi itasaidia watu kujua historia na magumu ambayo Muungano wetu umepitia kwa sababu hata katika baraza la mawaziri, kuna vitu nikiuliza vya kimuungano, watu wanakosa majibu. Vitabu  hivi vitasaidia kutupa uelewa kwani wengi wamezaliwa baada ya Muungano," amesema.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameipongeza timu iliyofanikisha uandishi wa vitabu hivyo ambavyo vitasaidia kuongeza uelewa kwa Watanzania na wageni.

"Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wamezaliwa baada ya Muungano, hivyo vitabu hivi ni nyenzo muhimu kusaidia watu kuufahamu muungano wetu," amesema.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema vitabu hivyo vinabeba historia kubwa ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa la Tanzania yakiwamo mafanikio na changamoto zake.

Amesema vitabu hivyo vikatumike kuwajengea uelewa watoto na watu wote ambao wamezaliwa baada ya Muungano ili waufahamu na kuulinda kikamilifu.

"Lakini pia tunao wajibu sisi kama taifa kuendelea kuwakumbuka na kuwaenzi viongozi wetu wote waasisi wa Muungano huu," amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo amesema kupitia vitabu hivyo, Watanzania watapata fursa kuuelewa Muungano kwa kuwa bado watu wengi hawana uelewa wa kutosha.

"Vitabu hivi vimeeleza mambo mengi sana ikiwamo wasifu na mambo ambayo yalifanywa na viongozi waliowahi kuhudumu kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais tangu mwaka 1964," amesema.

Amesema tangu Muungano uanze mwaka 1964 hadi leo, Makamu wa Rais 14 wamehudumu katika ofisi, tisa wakitoka Zanzibar na watano Tanzania Bara na kati ya hao, mwanamke ni mmoja tu kwa miaka yote 60 ya Muungano.