RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na wanyamapori waharibifu wanaovamia mashamba ya wananchi na kuharibu mazao wakiwamo tembo.
Ametaja moja ya mpango ni kuongeza ndege nyuki na kuimarisha vituo vya askari wa maliasili ili kurahisisha kazi ya kuwadhibiti.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Tunduru kwa nyakati tofauti ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku ya nne Mkoa wa Ruvuma, Rais Samia pia amezindua soko la madini Tunduru.
Rais Samia alitaja mikakati inayofanyika kuwa ni pamoja na kuongeza askari wa wanyamapori katika maeneo mbalimbali na kuwaongezea ujuzi askari wanyamapori wa vijiji ili washirikiane kuwadhibiti.
Alisema serikali imeweka magari ya doria katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo yanayorahisisha utekelezaji wa shughuli hiyo pamoja na ndege nyuki inayotumika kufukuza tembo.
“Tunajua kuna tatizo la tembo, lakini tumeanza kuchukua jitihada hizo na mengine yanafuatia, lengo letu ni kuongeza idadi ya ndege nyuki ili kufukuza tembo na kuimarisha vituo vya askari wa maliasili ili waweze kufanya kazi ya kuwafukuza,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema serikali inaendelea kuwashika mkono wakulima kwa kutoa ruzuku na kuongeza bei ya kununua mazao hadi kufikia Sh. 700 kwa kilo, ili kukuza sekta ya kilimo na kuwasisitiza kuongeza uzalishaji wa mazao.
Alimwagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo kushirikiana na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, kuhakikisha wanafufua kiwanda cha kubangua korosho kilichoko wilayani humo na kukitafutia mwekezaji mwingine baada ya yule wa zamani kushindwa kukiendesha.
“Tunataka kilimo kikue, kichangie katika pato la taifa, kwa kiasi kikubwa na tunauona mwelekeo. Kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu wananchi tufanye kazi kwa bidii,” alisisitiza.
Aliwaonya wakazi wa eneo hilo kuacha kuchoma moto mashamba, kwa kuwa kunasababisha uharibifu wa mazingira ikiwamo misitu, barabara na kuharibu taswira ya nchi na kuchochea athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Mkichoma moto mnaharibu misitu, lami ile ikipata moto inayeyuka barabara zinaharibika, sasa badala ya kuwaletea maendeleo pesa ileile inarudi tena kutengeneza barabara, tukaimarishe misitu inakuwa kazi kubwa.
“Eti nani aliwaambia kuwa ukichoma moto eneo kubwa ndio baraka ya biashara, haya mlishachoma moto, mlipata hiyo biashara? Basi acheni kuchoma moto,” aliagiza.
Aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa wanadhibiti uchomaji wa mashamba ovyo na kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kukuza kilimo.
Alisema kuwapo soko la madini kutawahakikishia wachimbaji wadogo bei nzuri ya bidhaa hiyo kutokana na ushindani utakaokuwapo.
Aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kama wanaona kuwa kuna haja ya kujenga soko lingine, wazungumze na sekta binafsi ili lijengwe kwa njia ya ushirikiano.
Aliwakumbusha vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao na kuchagua viongozi wanaowakilisha maslahi yao.
Alisema serikali itajenga hosteli za kukaa wanafunzi wasichana katika Jimbo la Tunduru Kaskazini kama mbunge wake, Hassan Kungu, alivyoomba.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa, alimwomba Rais Samia katika kuzuia usumbufu wa wanyamapori waharibifu ambao wamekuwa akivamia mashamba ya wanakijiji na kuharibu mazao, juhudi za kuwadhibiti ziongezwe.
Mbunge wa Tunduru Kusini, Idd Mpakate, alimwomba Rais Samia awasaidie kugawanya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya utawala wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru, Chiza Marando, alisema Soko la Madini, limejengwa kwa ushirika kati ya serikali na sekta binafsi na ujenzi wake umegharimu Sh. bilioni 1.4.
Alisema kati ya hizo fedha, wafanyabiashara wa madini wamechangia Sh. bilioni 1.085 na Halmashauria Sh.milioni 319. Kati ya fedha hizo Sh. milioni 288 ni thamani ya ardhi ya eneo lilijengwa jengo hilo.
Alisema ujenzi wa soko hilo utasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini kwa sababu lina vyumba vya kutosha kuweka wafanyabiashara wote katika eneo moja.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED