Sakata la utekaji, kupotea watu laibuka Bungeni

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:53 AM Aug 30 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

SAKATA la matukio ya utekaji, mauaji na kupotea watu limeibuliwa tena bungeni huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwaomba wananchi kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika wa mambo hayo.

Majaliwa aliyasema hayo jana bungeni katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Anatropia Theonest. Mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa serikali wa kuzuia vitendo hivyo,.

“Kuna matukio yanaashiria uvunjifu wa amani. Matukio  haya ni utekaji, mauaji na upoteaji wa watoto na yamekuwa na sura tofauti ikiwamo wivu wa kimapenzi lakini pia ushirikina na matukio mengine ya kutekwa na kuuawa watu yanayohusisha vyombo vya dola,” alisema mbunge huyo.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kabla ya kumpa nafasi Majaliwa kujibu swali hilo, alisema juzi alisimama Mbunge wa Nkasi, Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani, akizungumzia suala hilo na kwamba mambo hayo yanahitaji uchunguzi.

“Ukiyasema kwa ujumla haya maneno ya utekaji, mauaji, leo asubuhi nimesoma kuna mganga amezika watu zaidi ya 10 sasa wale ni vyombo vya dola?”

“Kila mwanadamu ana haki ya kuishi. Msiweke mazingira ya kuonesha kwamba kila anayepotea ni vyombo vya dola, kuna watoto, kuna mabasi wanapanda kule chini akidondoka njiani familia ikimtafuta utasema ni chombo cha dola kimemchukua? Wakati wote tunabidi tufanye hii kazi kama viongozi. Tukitumia  mihemko hatutoi nafasi kwa serikali kufanya kazi yake wakati huo huo hatutoi nafasi kwa jamii kuendelea kushiriki hili jambo.

“Waziri Mkuu labda utoe maelezo ya jumla kuhusu hilo lakini kuhusu swali sisi wote humu ndani ni viongozi na tunawakilisha wananchi tungependa wananchi wawe salama. Sasa ukisema mambo ya jumla jumla chukua nafasi kama kiongozi unaweza kushauri lakini usinyoshe vidole kwa kuwa huna uhakika,”alisema Spika.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema wanapolinda nchi ni wajibu wa Watanzania wote kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama  vyenye jukumu la kupokea taarifa mbalimbali zilizoonesha uvunjifu wa amani popote pale na jukumu lao wakishapokea taarifa ni kuhakikisha wanafanya uchunguzi. Uchunguzi utakapobaini waliotenda makosa wanachukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Alisisitiza kuwa, serikali imeendelea kusimamia misingi na kudhibiti mambo yanayotishia amani ya nchi na usalama wa raia na mali zao.

“Suala la ulinzi na usalama bado liko mikononi mwetu pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Jukumu letu ni kusaidia vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa taarifa zozote zile zinazoleta tishio la amani katika nchi ili vyombo vyetu vichukue tahadhari na hatua stahiki ili kuwabaini wale wote wanaosababisha kutokuwapo kwa amani katika nchi yetu,”alisema.

Majaliwa alimshukuru Spika kwa maelezo yake ya awali ili kuondoa upotoshaji unaoendelea kufanywa na kusababisha vyombo kushindwa kufanya kazi na kuwavunja moyo watu wanaofanya kazi ya ulinzi saa 24 ili kuhakikisha nchi inabaki salama.