Saa 72 za Makonda zilivyosimamisha usafiri Arusha

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:31 AM Jan 01 2025
Saa 72 za Makonda zilivyosimamisha usafiri Arusha

SAA 72 za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alizotoa kwa wageni na wakazi wa jijini hapa na viunga vyake kushiriki sherehe za kufunga na kuukaribisha mwaka 2025, zimesimamisha huduma za usafiri katika baadhi ya barabara ili kupisha shamrashamra hizo.

Makonda, alitangaza kuliteka kwa shangwe Jiji la Arusha kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 29 hadi 31, mwaka jana kwa burudani na matukio mbalimbali. 

Jana Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, kilitangaza barabara zilizofungwa kupisha mkesha huo kuukaribisha mwaka mpya na kutangaza njia mbadala kwa watumiaji wa barabara ili kuepuka usumbufu. 

Mkuu wa Kikosi hicho wa Mkoa huo,  Zauda Mohamed alizitaja barabara zilizofungwa kuwa ni ile ya kutoka mzunguko wa jengo la Ngorongoro Tower kuelekea ofisi za Jiji la Arusha na mnara wa saa.  

Nyingine ni makutano ya Barabara ya Goliondoi na Joel Maeda (maarufu Airtel) kuelekea mnara wa saa; makutano ya barabara ya Goliondoi na Uhuru (zilipo ofisi za Vodacom) kuelekea mnara wa saa.  

Barabara ya makutano ya TANESCO na Fire (Zimamoto) kuelekea mnara wa saa na makutano ya Barabara ya Kanisa na Nyerere kuelekea mnara wa saa. 

Kwa mujibu wa Zauda, kutokana na shangwe za kuuaga mwaka 2024, wananchi wanaotumia barabara za katikati ya jiji wanapaswa kuchagua njia mbadala. 

Alisema askari wa kikosi hicho watakuwepo kutoa mwongozo wa barabara ili kupunguza msongamano.