RIPOTI MAALUM: Ukeketaji wageuzwa kipato

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:03 AM Jul 29 2024
Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni- Ukonga jijini Dar es Salaam, Selemani Bishagazi, akitoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mpakani Sirari mkoani Mara kuhusu namna ya kuachana na mila kandamizi.
PICHA: ELIZABETH ZAYA
Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni- Ukonga jijini Dar es Salaam, Selemani Bishagazi, akitoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mpakani Sirari mkoani Mara kuhusu namna ya kuachana na mila kandamizi.

MAPATO makubwa wanayopata ngariba na wazee wa mila wakati wa sherehe za ukeketaji yanasababisha vita dhidi ya ukatili huo kuwa ngumu.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe wilayani Tarime, mkoani Mara hivi karibuni, umebaini ngariba hulipwa wastani wa Sh. 20,000 hadi 40,000 kwa kila msichana anayemkeketa, baadhi wakikeketa wasichana 150 hadi 200 kwa siku wakati wa msimu wa sherehe hizo za kimila.

Mwandishi wa Nipashe amebaini sherehe hizo hufanywa mwishoni mwa mwaka, zikichukua muda wa wiki mbili hadi tatu. Hivi sasa sherehe hizo zinafanywa katika miaka inayogawanyika kwa mbili tu.

Hata hivyo, sheria za Tanzania zinakataza kufanya utekeketaji na adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka 15.

Ngariba Wankyo Chacha, mkazi wa Kijiji cha Mpakani, Kata ya Sirari, wilayani Tarime anathibitisha amekuwa analipwa kwa kufanya ukeketaji, malipo ambayo hugawana na wazee wa mila.

"Ni kweli kuna malipo unapofanya kazi hii, lakini sisi (ngariba) huwa tunasikiliza na kutekeleza maagizo ambayo tunapewa na wazee wetu wa mila kwa sababu wao ndio viongozi katika koo, wanaheshimika toka enzi na enzi.

"Na hata kile kinachopatikana baada ya kazi huwa ni lazima kigawanywe sawa kwa wazee wa mila na ngariba kwa kuwa wao ndio waratibu wakuu wa kazi hii," anasema Wankyo.

Ngariba huyo ambaye anadai hajui kwamba anavunja sheria kwa kukeketa wasichana, anataja changamoto kubwa kwake baadhi ya watoto kuogopa na hivyo kujikuta anatumia muda mrefu tofauti na unaopangwa na wazee wa mila.

"Unaweza kuletewa mtoto ambaye ni mwoga, kila ukitaka kumfanyia, analia. Hivyo, inabidi utulie uzungumze naye kwanza. Ukikutana na watoto wengi wa namna hiyo wanakupotezea muda, badala ya kukeketa 150 kwa siku, unajikuta umekeketa 100 au badala ya kumaliza kazi ndani ya wiki mbili unajikuta unakwenda hadi wiki tatu au zaidi.

"Gharama ya kufanya kazi hiyo kwa kila mtoto ni Sh. 20,000, kwa siku unaweza kuwafanyia watoto 100 au 150, unapata fedha nyingi," anasema Wankyo.

Mmoja wa wazee wa mila katika Kijiji cha Nyamrenge, Kata ya Sirari, Francis Mwita, anatetea ukeketaji katika jamii yao kwa maelezo kwamba mafundisho ambayo huambatana na shughuli hiyo ya ukeketaji yanasaidia kujenga wasichana katika maadili mema.

"Suala la tohara tuwaachie wazee, wenyewe ndio watajua watamaliza vipi, lakini ukiliingilia unaokosea. Huko wasituguse kabisa kwa sababu ndio mila tuliyozaliwa nayo na tumerithi kutoka kwa wazee wetu.

"Watoto kukeketwa kuna maana tatu: Mtoto wa kike kabla ya kukeketwa, bibi zake huwa wanamwambia hatakiwi kutembea na mwanamume kwa sababu akifanya hivyo siku, akienda kukeketwa hatakeketwa kwa sababu atajulikana kwamba tayari ameshatembea na mwanamume na analeta aibu katika familia.

"Pili, akishakeketwa anaambiwa asikumbatiwe na mwanamume wala kuguswa kwenye kifuani kwa sababu akifanya hivyo, kuna miiko ambayo hatafanyiwa akigundulika. Kwa hiyo, inasaidia ajilinde.

"Tatu, anaambiwa akishaolewa hatakiwi kutembea nje ya ndoa kwa sababu kutokana na miiko aliyofanyiwa atagundulika. Hiyo miiko inasaidia watoto kuwa na maadili.

"Hivyo, tunashauri serikali itafute njia nzuri ya kumaliza hili polepole na si harakaharaka kama wanavyotaka.

"Hii nguvu inayotumika kutaka kuzuia watoto kukeketwa itachangia wawe huru zaidi kufanya mambo ya ajabu kwa sababu wanafahamu kwamba hata wakifanya hivyo, hakuna mtu atajua lakini endapo wataendelea kukeketwa wataizidi kuogopa na hawataharibikiwa," Mzee Mwita anasema pasi na kuzingatia ukeketaji unakiuka sheria za nchi na ni ukatili dhidi ya wasichana.

Ester Wambura (21), mkazi wa Forodhani, kijijini Mpakani, Kata ya Sirari anasimulia alivyolazimishwa kukeketwa na wazazi wake, akidai walimtishia kwamba asipokeketwa, angetengwa na asingepata mwanamume wa kumuoa.

"Nikiwa darasa la sita, wazazi wangu waliniambia ninatakiwa kukeketwa, binafsi sikutaka lakini wazazi waliniambia ni lazima kwa sababu nitatengwa na itakuwa aibu kwa familia na wakanitishia sitapata mwanamume wa kunioa, hivyo nikakubali.

"Baada ya kukeketwa alijitokeza mwanamume anataka kunioa hata kabla sijamaliza elimu ya msingi. Kwa kutaka kuwaridhisha wazazi wangu, sikutaka kufanya vizuri hata kwenye mitihani yangu ya darasa la saba ili niolewe, lakini ninaposimulia haya leo, nina watoto wawili na mume ameniacha.

"Ninajutia uamuzi wangu, ninatamani nisingekeketwa labda hao wanaume wasingeshawishika kunifuata na ningeweka nguvu zangu kwenye masomo na huenda ningekuwa na maisha mazuri baadaye," Ester anajuatia uamuzi wake.

Elizabeth Joseph, mkazi wa Kijiji cha Bondeni, Sirari, anasema haamini kama kweli ukeketaji kwa sasa upo kwa ajili ya mila, bali kwa maslahi ya watu, akiwa na hoja kwamba wapo wanawake waliokeketwa katika ya eneo anamoishi, lakini wameachwa na waume zao, kama ilivyo kwa mtangulizi wake - Ester.

"Tunasema wanaendekeza ukeketaji kwa sababu hivi sasa hatuwaelewi wanaume, wanataka wanawake wakeketwe lakini wakiwaona hao waliofanyiwa hivyo, hawawataki tena. Tuna ushahidi wa wanawake wengi waliokeketwa ambao wameachika, wanasema wanataka wanawake wasiokeketwa.

"Tunataka serikali iongoze nguvu kukemea jambo hili lisifanyike kabisa kwa sababu kuna watu wanaangalia maslahi yao wenyewe wakati watoto wanaumia. Binafsi nimekataa watoto wangu wasikeketwe, ninataka wasome kwa uhuru mpaka wachoke wenyewe," anasema Elizabeth.

Msichana aliyekimbia kukeketwa mwaka 2020 (jina tunalo), anasema kuwa hadi sasa wazazi wake hawataki arejee nyumbani na anaishi. Hivi sasa msichana huyo (17) analelewa katika kituo kinachopokea watoto waliokimbia kukeketwa kilichoko wilayani Serengeti, mkoani Mara.

"Mimi nilikimbia wakati maandalizi yote yameshafanyika na siku iliyokuwa inafuata, nilitakiwa nifanyiwe, wazazi walikuwa wamenunua kila kitu kwa ajili ya sherehe na watu walikuwa wamealikwa.

"Sikuonesha dalili yoyote ya kukataa wala kuwaabishia, nilikubali huku moyoni nikipanga namna ya kukimbia. Huwezi amini, alfajiri sana kama saa 10 hivi, nikajifanya kama ninawahi kudamka kwa ajili ya maandalizi, kumbe ndio ninatoroka.

"Nguo nilizobeba hazikuzidi tatu na nilizipitisha dirisha la nyuma ya nyumba. Nikatokea mlangoni, nikiwa nimebeba ndoo kama ninakwenda kuchota maji, nikazunguka nyuma ya nyumba kuchukua hizo nguo na ndoo nikaiacha palepale, nikaondoka taratibu kwa kunyata huku nimejitanda kanga mpaka barabarani. Nikapanda bodaboda mpaka hapa kituoni.

"Kipindi hicho nilikuwa ninasoma darasa la saba. Baada ya msimu wa ukeketaji kuisha, Januari 2021 nikapiga simu nyumbani, hawakutana kunisikiliza, nikaenda na mwalimu anayetusaidia hapa, naye hawakumsikiliza.

"Madai yao wanasema aibu niliyosababisha kwa familia ni kubwa. Nikakubaliana na matokeo, nimejifunza ushonaji kwa msaada wa kituo hiki. Sasa ninashona nguo za wateja, ninapata fedha zangu mwenyewe, ninaamini nikipata fedha za kutosha nitaanza kuwasaidia watakubali nirudi nyumbani," anasema.

Rhobi Samweli, Mkurugenzi wa Kituo cha Hope for Girls and Women in Tanzania anakolelewa msichana huyo wilayani Serengeti, anasema baada ya serikali na wadau kuweka nguvu zaidi ya kuzuia ukeketaji, ngariba na wazee wa mila wamebadili mbinu; wanawavalisha watoto wa kike nguo za kiume na kofia na kuwachanganya kundi moja na wavulana wanaopelekwa kufanyiwa tohara kimila.

Mkurugenzi huyo pia anasema ukeketaji unafanyika kwa miaka inayogawanyika kwa mbili tu, wakiamini miaka hiyo inakuwa na baraka, mavuno mengi na haina mikosi.

Rhobi pia anasema kuwa kutokana na kukusanya fedha nyingi, wazee wa mila wakati wa msimu wa ukeketaji hufikia hata hatua ya kukodi ngariba kutoka nchi jirani - Kenya.

"Wanajua ngariba atalipwa kutokana na kazi hiyo. Kwa mfano, kama wamepanga kila mtoto anakeketwa kwa Sh. 40,000, wanaganawana nusu kwa nusu.

"Na hii ndio sababu hasa ya kuendeleza ukatili huu. Ukeketaji huu ni maslahi. Ndio maana kabla ya msimu wa ukeketaji kuanza wanaandaa orodha ya majina ya watoto wa kike ambao watakuwa tayari kukeketwa. Wanapita kila ukoo kuhamasisha wapelekewe majina.

"Kwahiyo, kabla ya ukeketaji kuanza wanakuwa na orodha ya watoto wangapi wanaokeketwa, na wengine wanapowakeketa wanawaozesha kwa wazee wenye kipato kizuri ili wapate fedha za kusaidia kutatua changamoto zao," anasema Rhobi. 

Mkurugenzi huyo anasema zoezi la kuhamasisha watoto wapelekwe kukeketwa msimu wa ukeketaji unapokaribia, hufanywa kwa umakini mkubwa; katibu wa mila huzunguka na ngariba kuorodhesha majina ya wasichana.

"Na katika kila nyumba ambako wanafahamu kuna msichaka ambaye hajakeketwa, huwa wanaweka ulinzi wao kwa siri ili kuhakikisha haendi popote au kukimbia.

"Kwa mfano, sisi tuna nyumba ambayo tunaitumia kusaidia kuhifadhi wasichana ambao wanakimbia kukeketwa, tunaiita ‘nyumba salama’. Kikifika kipindi cha ukeketaji, wazee wa mila wanaweka ulinzi wao kuhakikisha wasichana hawaji katika nyumba hii.

"Huwa tunafanya kazi na bodaboda ambao huwa tunawaelimisha kwamba wanapoona mtoto anataka kukeketwa wasaidie kumtorosha, lakini kutokana na nguvu ya hawa wazee wa mila, kuna wakati na wao (bodaboda) huwa wanashindwa namna ya kuwaondoa wasichana kutokana na ulinzi mkali unaowekwa na hao wazee," anasema mkurugenzi huyo. 

Rhobi anadai kuwapo vitisho dhidi yake kutoka kwa wazee wa mila kutokana na kusaidia wasichana wanaotoroka kukeketwa.

"Huwa wananiambia 'tutakuua', wanasema 'hata ukija na wenzako gari lenu litapinduka mfe' na wananitukana matusi, wanasema tunawaharibia kibarua chao," anadai Rhobi na kubainisha kuwa hadi sasa, kitu chake kina wasichana 104 kiliowapa hifadhi katika 'nyumba salama' baada ya kukimbia kukeketwa.

Hoja ya Rhobi kuhusu ukeketaji kugeuzwa 'duka' la ngariba na wazee wa mila, inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpakani, Kata ya Sirari, Julius Mwita, anayetaja malipo kwa ajili ya mtoto kukeketwa ndicho kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya ukeketaji katika eneo lao.

"Zamani watoto wa kike wakikeketwa walikuwa wanavalishwa vitenge, baada ya kuona Jeshi la Polisi linafuatilia vitendo hivi, wanachanganya watoto wa kike na wa kiume kwenye ule msafara wa tohara, hivyo ni vigumu mgeni kufahamu, wasichana wengi wanaokeketwa ni wa umri wa balehe," anasema Julius.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga anakosa adhabu iliyopo kisheria dhidi ya wanaokeketa wasichana, akiwa na hoja kwamba ni ndogo na inatolewa kwa waliotenda ukatili huo kwa watoto tu; hakuna adhabu iliyotajwa kisheria kwa anayekeketa mwanamke mwenye umri wa kuanzia miaka 18.

Inaporejewa Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, kifunngu cha 69A(1) kinaelekeza: "Mtu yeyote ambaye ni mwangalizi, ana wajibu au usimamizi wa mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18, akimtesa au akimtelekeza mtu huyo au akisababisha tohara kwa mwanamke au akimtahiri au kusababisha tohara hiyo ifanyike au kusababisha mtu huyo adhalilishwe, ateswe, au atelekezwe kwa namna ambayo itamsababishia maumivu au madhara kwa afya yake, pamoja na maumivu au kuharibu uwezo wake wa kuona, kusikia au kiungo chochote cha mwili au akili, atakuwa ametenda kosa la ukatili kwa mtoto.

Kifungu cha 169A(2) cha sheria hiyo, kinaelekeza kuwa mtu yeyote ambaye atapatikana na kwa kutenda kosa la aina hiyo kwa mtoto atawajibika kwa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka mitano na kisichozidi miaka 15 au faini isiyozidi Sh. 300,000 au vyote kwa pamoja, na kuamriwa kulipa fidia ya kiasi kitakachoamuliwa na mahakama kwa yule aliyetendwa kosa hilo.

Dk. Anna anasema: "Tukiangalia madhara yanayowapata hao wasichana ikiwamo ugumba, kupata fistula, kupoteza watoto au kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua, unaona hakuna haja ya kufanya ukeketaji.

"Kuna haja kuunganisha nguvu kuanzia ngariba, serikali, asasi za kiraia na jamii kuwa na sauti ya pamoja kuondoa mgawanyiko uliopo wa wanaotaka ukeketaji uendelee na wanaotaka usiendelee.

"Sisi LHRC kwa kushirikiana na Mtandao wa Kupinga Ukeketaji Tanzania, tuliwahi kukutanisha wazee wa mila na viongozi wa dini. Kwa kweli mwaka ule ukeketaji ulishuka sana kwa sababu makundi hayo yana watu wenye nguvu katika jamii, wakisema 'hapana' na wananchi wanasema 'hapana'".

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu, anasema jamii anayoongoza inaona ukeketaji si tatizo; ndio sababu hairipoti kwa vyombo vya dola matukio ya ukatili huo.

"Wanaripoti ubakaji na ulawiti, lakini tukio la msichana ameshikwa na kupelekwa kukeketa hawaoni kama ni tatizo na huwasikii wanakwenda kuripoti kwenye vyombo vya dola," anasema Kanali Surumbu.

Kiongozi huyo wa wilaya anasema kuwa hivi sasa wanaweka nguvu kubwa kuelimisha ngariba na wazee wa mila kuachana na ukeketaji.

"Kuna kipindi tuliandaa njia mbadala ya kusaidia wazee wa mila kupata kipato badala ya kutegemea ukeketaji, waliifuata kwa muda mfupi halafu baadaye wakarudia tena kufanya ukeketaji, bado tunaendelea kuwaelimisha," anasema Kanali Surumbu. 

Mkuu wa Kituo cha Polisi Sirari, Rashid Chamwi, anasema jitihada za kudhibiti vitendo vya ukeketaji vinakwamishwa na mbinu mpya, hasa wazee wa mila kushirikisha ngariba kutoka nchi jirani.

"Tumepata malalamiko kwa wenzetu wa nchi jirani - Kenya, wanasema wasichana wanadhibitiwa kukeketwa huko kwao, wanaletwa nchini kwetu kuja kukeketwa, lakini hiyo si kwao tu, na sisi tukiwadhibiti huku wanakimbilia nchini jirani kwenda kufanyia huko. Ndio changamoto tunayotafuta mbinu ya kupambana nayo," anasema Chamwi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, mikoa yenye kiwango kikubwa cha ukeketaji kwa sasa ni Arusha (asilimia 43), Manyara (asilimia 43), Mara (asilimia 28), Singida (asilimia 20), Tanga (asilimia 19), Dodoma (asilimia 18), Iringa (asilimia 12), Morogoro (asilimia 10), Kilimanjaro (asilimia tisa), Njombe (asilimia saba), Pwani (asilimia tano) na Mbeya (asilimia tatu). 

Waziri Dorothy anasema wizara inaendelea na utekelezaji mkakati wa kupunguza vitendo hivyo hadi asilimia tano ifikapo 2025, mwaka ambao ni ukomo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.