Ridhiwani Kikwete agawa majiko ya gesi 118 kwa mama lishe Chalinze

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:08 PM Dec 10 2024
Ridhiwani Kikwete agawa majiko ya gesi 118 kwa mama lishe Chalinze
Picha:Mpigapicha Wetu
Ridhiwani Kikwete agawa majiko ya gesi 118 kwa mama lishe Chalinze

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, amegawa majiko ya gesi 118 kwa mama lishe wa kata 15 za jimbo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya ugawaji wa majiko hayo, Ridhiwani amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutunza mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

"Sasa mtakwenda kupika chakula kwa haraka na kwa usafi. Hii itasaidia sana shughuli zenu, na kwa pamoja tutamuunga mkono Mheshimiwa Rais katika uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia," amesema Ridhiwani.

Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Dawati la Jinsia wa Halmashauri ya Chalinze, Recho Mnguruta, amesema majiko hayo yatasaidia wanawake wajasiriamali kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa, nishati ambazo siyo rafiki kwa mazingira na zina changamoto nyingi.

Lilian Skawa, mmoja wa walengwa kutoka Msata, ametoa shukrani kwa Mbunge huyo, akisema majiko hayo yataimarisha shughuli zao za upishi.

"Kipindi cha mvua tulikuwa tunapata changamoto ya mkaa, mara nyingine unakuwa umelowa, na hii ilichelewesha kazi zetu. Sasa tutapika kwa wakati, kwa usafi, na kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi," amesema Lilian.

Hatua hiyo ya ugawaji wa majiko ya gesi inatajwa kuwa suluhisho muhimu kwa changamoto zinazowakabili mama lishe, hasa wakati wa mvua, huku ikichangia jitihada za kupunguza ukataji miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.

Mbunge Ridhiwani amesisitiza kuwa juhudi hizo zinaonyesha dhamira ya serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi na salama, huku wakilinda mazingira kwa vizazi vijavyo.