Polisi yaonya waganga wa jadi matukio ubakaji, ulawiti

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:49 AM Sep 05 2024
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, kuhusu operesheni mbalimbali za kudhibiti uhalifu zinazoendelea kufanywa na jeshi hilo.
PICHA: JUMANNE JUMA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, kuhusu operesheni mbalimbali za kudhibiti uhalifu zinazoendelea kufanywa na jeshi hilo.

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekutana na waganga wa tiba mbadala 80 na kuwaonya kuacha kufanya ramli chonganishi kwa kuwapa masharti wateja wao kuwa ili wafanikiwe kibiashara na kupata utajiri, wajihusishe na vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto.

Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya jeshi hilo katika kushughulikia matukio ya ukatili dhidi ya makundi hayo kwa mujibu wa sheria.

Muliro alisema juzi Jeshi la Polisi lilifanya kikao na waganga hao wanaojulikana kama wa tiba mbadala  kwa lengo la kuwaelimisha kuacha kujihusisha au kufanya ramli chonganishi.

“Kuacha tabia ya kuwapa masharti baadhi ya wateja wao kuwa ili wafanikiwe katika biashara na kupata utajiri, lazima wafanye vitendo viovu vya kuwalawiti au kuwabaka watoto.

“Jeshi la Polisi limetoa tahadhari na kuwaonya vikali waganga wanaofanya hivyo kuwa watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.

Kuhusu kusimamia mifumo ya kisheria na utekelezaji wa taarifa ya Tume ya Haki Jinai, Kamanda Muliro alisema jeshi hilo limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya kihalifu ambao baadhi yao wamepatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kupewa adhabu.

“Jeshi la Polisi limekuwa likichukizwa sana na vitendo vya ubakaji na ulawiti na katika hatua hiyo, washtakiwa katika kesi 16 kuanzia za makosa ya kubaka na kulawiti zilizosikilizwa kati ya Julai hadi Agosti, mwaka huu, walihukumiwa adhabu za vifungo cha maisha jela akiwamo Boniphace Paul (24), mkazi wa Mbezi kwa Musuguri,” alisema.

Kamanda Muliro alisema mshtakiwa mwingine, George Godfrey (21), mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, alikamatwa eneo la Coco Beach na kufikishwa mahakamani kwa unyang’anyi wa kutumia silaha ambako baada ya shauri lake kusikilizwa, alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro alisema Septemba 3, mwaka huu, saa 2:00 usiku, jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa maeneo ya Tanganyika Parkers, Kawe, kulikuwa na watu wawili waliokuwa na mapanga wakitishia na kuwapora wapita njia.

“Ufuatiliaji wa polisi ulifanyika haraka na kuwakuta watu hao, walipotaka kukamatwa walikaidi na kutoa mapanga kutaka kumdhuru mmoja wa askari, ambaye alijihami kwa kupiga risasi hewani.

“Baadaye alipokuwa katika hatari kubwa ya kudhuriwa, alimjeruhi kwa risasi mtuhumiwa mmoja, Festo Maricha (27), mkazi wa Mbezi Luis na mwenzake ambaye hakufahamika jina alikimbia. Mtuhumiwa amepelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu,” alisema Muliro.

Kamanda Muliro alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali zitazosaidia mkakati wa kuzuia zaidi vitendo vya kihalifu ili Dar es Salaam iendelee kuwa salama.