PM: Uvuvi waingiza mapato trilioni 2.9/-

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:54 AM Sep 12 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akipata maelezo kutoka kwa Mratibu wa FISH4ACP, Hashim Muumini, kuhusu teknolojia ya ukaushaji wa dagaa. Pembeni ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akipata maelezo kutoka kwa Mratibu wa FISH4ACP, Hashim Muumini, kuhusu teknolojia ya ukaushaji wa dagaa. Pembeni ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema sekta ya uvuvi inaingiza mapato ya Sh. trilioni 2.94 kwa mwaka na imekuwa ikikua kwa wastani wa asilimia 1.9.

“Wastani wa uzalishaji wa samaki kwa mwaka hapa nchini unafikia tani 472,579, huku 429,168 sawa na asilimia 91 zikitokana na uvuvi wa kawaida wa kutumia vyanzo vya asili ndani ya bahari, mito na maziwa na tani 43,411 sawa na asilimia tisa zikitokana na ufugaji wa samaki.”

Alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS), wanaohusika na masuala ya uvuvi, bahari, maziwa na mito ulioanza jana jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu alisema kila siku watu 230,000 wanajishughulisha na uvuvi mdogo na Watanzania milioni sita wamepata ajira zisizo za moja kwa moja kwenye sekta hiyo. “Uvuvi mdogo mdogo unachangia zaidi ya asilimia 95 ya mavuno yote ya samaki nchini,” amesema.

Akielezea fursa za uwekezaji kwenye ufugaji wa samaki, alisema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuendeleza sekta hiyo kutokana na rasilimali kubwa za maji ilizonazo ikiwa ni pamoja na Bahari ya Hindi, maziwa, mito, mabwawa mengi ya asili na yaliyojengwa na binadamu.

 “Eneo Maalum la Kiuchumi la Tanzania ni fursa kubwa ya uwekezaji kupitia ununuzi wa meli za uvuvi, uwekezaji wa huduma za meli, usambazaji wa vifaa vya uvuvi, usambazaji wa chakula (maji, chakula na matunda), kuongeza thamani na usindikaji, utafiti na ulinzi wa baharini na angani.”

Alizitaja fursa nyingine za uwekezaji kuwa ni pamoja na uvuvi wa kina kirefu kwa ajili ya samaki aina ya tuna; kilimo cha mwani; uzalishaji wa vifaranga na chakula cha samaki.

Akielezea matarajio ya mkutano huo, Waziri Mkuu amesema mkutano huo utatoa mwongozo wa kimkakati kwenye vikao vya juu vya maamuzi vya Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki ili kuboresha usimamizi wa bahari, uvuvi na ufugaji endelevu wa samaki.

Amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono malengo ya umoja huo hasa katika kukuza uchumi wa bluu na maendeleo endelevu. “Uamuzi huu utasaidia kuimarisha malengo ya umoja wetu na kuboresha ustawi wa nchi wanachama pamoja na wananchi wake. Umoja huu ni miongoni mwa majukwaa ya msingi sana yanayoweza kuchangia mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu ya Tanzania.”

Umoja wa Nchi za Afrika, Karibian na Pasifiki (OACPS) unajumuisha nchi wanachama 79 ambapo 48 kati ya hizo zinatoka Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, nchi 16 zinatoka Caribbean na nchi 15 zinatoka Pasifiki. Umoja huu ambao unalenga kuchochea maendeleo endelevu, kuondoa umaskini na kukuza fursa za kibiashara miongoni mwa wanachama wake umetokana na kundi la nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (ACP) ambalo lilianzishwa kwa makubaliano ya Georgetown ya mwaka 1975.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema umoja huo ni kiungo muhimu cha OACPS katika kukuza ushirikiano kati ya nchi wanachama na usimamizi wa rasilimali za bahari.