MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametangaza juu ya ujio wa ndege mpya ya abiria kesho, huku akiwataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuipokea ndege hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake leo Machi 25 jijini Dar es Salaam, Chalamila ndege hiyo aina ya Boing B 737-9 MAX ina uwezo wa kubeba abiria 181 na hivyo kuwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali.
Amesema kuwa hayo ni mafanikio na maendeleo ya nchi yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba Serikali iko katika juhudi za kuboresha usafiri wa anga nchini na hivyo kuitambulisha Tanzania kimataifa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo, tangu Rais Samia aingie madarakani, hiyo ni ndege ya tatu kununuliwa na Serikali kwani tayari ndege mbili zilishawasili ikiwemo ile ya abiria, pamoja na ndege ya mizigo.
“Nawaalika wananchi wote, viongozi wa dini, viongozi mbalimbali wa serikali tushirikiane kwa pamoja kupokea ujio wa ndege hiyo” amesema Chalamila.
Akizungumza na katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi akisema: “Katika miaka mitatu, Serikali imenunua ndege tano.”
Matinyi aliongeza kuwa: “kati ya ndege hizo, tatu ni za masafa ya kati, ambazo ni Airbus A220 mbili; Boeing 737 Max9; Boeing 767-300F na Dash 8 Q-400; na zote zinaendelea kutoa haduma."
Aidha, alisema kuwa ndege mbili zaidi zinatarajia kuwasili mwezi huu na Aprili huku akibainisha kuwa Boeing 737 Max9, ndiyo itatangulia kuwasili ikifuatiwa na Boeing 787-8.
Kwa mantiki hiyo, Matinyi ameusifia uwekezaji huo wa serikali huku askiema: “…sasa ATCL ina jumla ya ndege za abiria 12 na moja ya mizigo, ambazo zinazohudumia vituo 24; kutoka vituo 19 vya mwaka 2021, na inatarajiwa vitaongezeka vingine.”
Mbali na hilo, Msemaji huyo wa serikali alisema kuwa kutokana na mafanikio hayo, ATCL imefanikiwa kuongeza abiria kutoka 537,155 mwaka 2021 hadi 1,070,734 mwaka jana.
Lakini pia imezewa kuongeza usafirishaji wa mizigo kutoka tani 1,290 mwaka 2021 hadi 3,561 2023 huku miruko ikiongezeka kutoka 10,550 mwaka 2021 hadi 17,198 mwaka 2023.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED