NACTVET yaelimisha wanafunzi wa sekondari Manispaa ya Tabora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:05 PM Apr 25 2024
Wanafunzi wa Sekondari Tabora.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wanafunzi wa Sekondari Tabora.

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Kanda ya Magharibi, limewapatia elimu wanafunzi 5,000 katika shule za sekondari 20 za Manispaa ya Tabora kuhusu kazi za Baraza, taratibu na miongozo mbalimbali ya kujiunga na vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.

Akizungumza na baadhi ya wanafunzi, Meneja wa NACTVET Kanda ya Magharibi, Faraja Makafu amesema, kampeni hiyo imelenga kuondoa changamoto wanazopata wanafunzi wakati wa kuomba kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi mara baada ya kuhitimu masomo yao ikiwemo changamoto ya kudahiliwa katika vyuo na programu zisizo na ithibati ya Baraza. 

“Uzoefu wetu na maoni toka kwa wadau wetu mbali mbali umetufanya tuanzishe kampeni ya Kanda kwa kanda ili kuwasaidia wanafunzi kufanya maamuzi na machaguo sahihi  wakati wa kuomba vyuo. Wanafunzi wanapaswa kuomba udahili  kwa usahihi na kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa ili waweze kutimiza ndoto zao”,  alitamatisha  Faraja.

Aidha, Meneja huyo wa Kanda amewataka wanafunzi hao kusoma kwa makini kitabu cha mwongozo wa udahili ambacho kinapatikana  katika tovuti ya Baraza (www.nactvet.go.tz) kwani  kina maelezo ya kina ya  hatua kwa hatua hadi  kukamilisha udahili wa wanafunzi katika vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Kwa upande wao, wanafunzi hao kwa nyakati tofauti wameshukuru hatua ya  NACTVET kuanzisha zoezi la  kuwapatia wanafunzi  Elimu hiyo muhimu kwao na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wengine kwa kuwaeleza  umuhimu wa kuzingatia taratibu na miongozo pindi watakapoamua kujiunga na vyuo mbalimbali.

Kampeni ya uelimishaji wanafunzi wa shule za sekondari za Kanda ya Magharibi, mkoani Tabora imeanza Aprili 22, 2024 na itafikia tamati mnamo Mei, Mosi, 2024, ambapo miongoni mwa shule zilizokwishatembelewa  ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Wavulana Milambo, Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora, Shule ya Sekondari Themi Hill, Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora, Shule ya Sekondari Ipuli, Shule ya Sekondari Cheyo, Shule ya Sekondari Isevya na Shule ya Sekondari Mihayo.