NOVEMBA 12, 2024 Nipashe ilichapisha habari kuhusu kikundi cha vijana wanaojiita Maronjoo, kuwa tishio kwa wananchi wa Kijiji cha Churuku, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, kinachodaiwa kufanya uhalifu, kudhalilisha na kujeruhi watu.
Kikundi hicho ambacho kinadaiwa kutumika kuchunga na kulinda mifugo porini, kimekuwa kikifanya matukio hayo mara kwa mara.
Hata hivyo, matukio hiyo yameibuka tena katika Kata ya Jangalo hasa Kijiji cha Mlongia wilayani humo na kumlazimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma George Katabazi, kwenda kuzungumza na wananchi na kukabiliana na kikundi hicho.
Kamanda Katabazi alisema “Mimi nikiwa Kamanda wa Polisi Dodoma hiyo biashara ya Maronjoo ni mwisho tutahakikisha hao vijana wote wanakamatwa na tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria, nimemuelekeza Mkuu wa Polisi wa Wilaya hakuna kulala ahakikishe wote wanakamatwa.”
Alisema tayari kuna vijana wamefikishwa mahakamani na waliobaki pia wakamatwe.
“Tatizo lililokuwepo watu wanatoa taarifa kituo cha polisi lakini mlikuwa hamtoi ushahidi, polisi tutajitahidi kuwakamata sisi hatufungi watu, sasa tunawakamata tunafanya kazi nzuri wanafikishwa mahakamani ushahidi upo, lakini unafika wakati wa kutoa ushahidi hamfiki mnaogopa,” alisema.
Alisema ni muhimu wananchi kutoa ushahidi, kwa kuwa Mahakama haiwezi kufunga mtu bila kuwapo na ushahidi na vijana watakapohukumiwa kifungo jela hawatarudia.
WANANCHI WAFUNGUKA
Mkazi wa Mlongia, Fahma Hamis, alisema hawana amani wananchi hasa wanawake wanabakwa wakiwa shambani na kuporwa vitu walivyonavyo ikiwamo sim una fedha.
“Tunaomba kituo cha polisi kiwepo hapa, kutoka hapa hadi mashambani ni kilometa zaidi ya 50 ambako Maronjoo wanakuwepo huko wamejificha, wale watu ni hatari unaweza kwenda na ukamanda wako ukafyekwa na panga.”
“Kinachosababisha wawe na akili za kikatili hawa vijana wanakunywa pombe na kuvuta bangi zinauzwa hapa kama mchicha Kijiji cha Mlongia, tunaporwa vitenge tulivyovaa wanasema hiki ndo kizuri tunaenda kuchungia na anakubaka anakwambia ukienda kusema kesho ukija nakumaliza,”alisema.
Mwenyekiti wa Kijiji, Songolo alisema wanateseka wanashindwa kuishi kwenye maeneo yao na kwamba ujio wa Kamanda kwenye eneo hilo amefarijika sana.
“Hawa wananchi wamekuja kumuona Kamanda aeleze namna atakavyookoa maisha yao maana kuna shida kubwa sana kwa Walonjoo wamefikia hatua wanakata hadi wanawake matiti,” alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kujengewa kituo cha polisi maana eneo walipo ni zaidi ya Kilometa 40 kwenda Kituo cha Mrijo wilayani humo.
“Hawa vijana wanatembea na silaha kama sime wamejifunga mashuka, hili nitatizo kubwa kuna watu wamejeruhiwa na hata kuna wengine wamewahi kupoteza maisha kwa kushambuliwa na kundi hili,”alisema.
Mwaka jana, Nipashe ilipata taarifa ya kuwapo kwa tukio la mauaji ya mtu mmoja na wengine watatu kujeruhiwa na kundi hilo na kusababisha wananchi wa eneo hilo kuhofia usalama wao.
Mmoja wa wananchi ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema kundi hilo limekuwa ni kero kwa wananchi wa kijiji hicho hali inayosababisha waishi maisha ya hofu.
“Hawa vijana maisha yao ni porini na kulala kwenye mazizi ya ng’ombe, ukiwaona wamejifunga mashuka ya kimasai lakini sio wamasai ni vijana wakirangi lakini matukio wanayofanya yamekuwa tishio, wakiwa na vurugu za kutofautiana huko wanakuja kijijini kama kulipiza kisasa,” alisema.
Mmoja watu waliojeruhiwa na kundi hilo, Athuman Makha, alikutana na kikundi cha vijana takribani 30 ambao walikuwa na mapanga na hadi leo hajui tatizo ni nini.
“Wamenishambulia wamenivunja mkono na mguu kama unavyoona umetolewa, hapa shavuni na mikwaruzo maeneo mengine ya mwili, sasa hadi sasa mbona sisikii kama kuna watu wamekamatwa, mbona kimya naomba serikali ichukue hatua,” alisema.
Naye, Shariff Makha, alishambuliwa na kundi hilo akiwa amelala alisikia watu wakibomoa nyumba yake.
Kadhalika, Abdi Saidi, alisema alisikia kelele kwa jirani yake usiku akiwa amelala na kulazimika kutoka ili kwenda kujua kuna tatizo gani na alipofika alikuta watu wengi wakiwa kimshambulia jirani yake na alipohoji kwanini wanafanya hivyo, mmoja wa vijana hao alimkimbilia na kumkata na panga mgongoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED