Mwamposa atabiri mambo makubwa mashindano ya pikipiki Arusha

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 08:24 PM Jul 13 2024
Mwamposa atabiri mambo makubwa mashindano ya pikipiki Arusha
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwamposa atabiri mambo makubwa mashindano ya pikipiki Arusha

MTUME na Nabii, Boniface Mwamposa, ametabiri mambo makubwa kwenye mashindano ya pikipiki mkoani Arusha yatakuwa ni mashindano ya kuvutia zaidi barani Afrika na dunia.

Mwamposa ameyasema hayo leo baada ya kutembelea viwanja vya Lakilaki Kisongo ambapo yanafanyika mashindano ya pikipiki ya Samia Motocross championship akiwa na Mkuu wa mkoa Arusha, Paul Makonda.

Mashindano hayo yanafanyika kesho Julai 14 mwaka huu na mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha Sh milioni 10, mshindi wa pili Sh milioni saba  na mshindi wa tatu ataondoka na Sh milioni tano.

Amesema uwanja huo ambao unaonekana ni wa pili kwa ubora Afrika Mashariki utakwenda kuwa wa kwanza kwa Afrika Mashariki na Afrika.

"Vijana ambao wanatoka katika mashindano haya wataenda kufanya vizuri katika mashindano ya duniani ya pikipiki ikiwemo yanayokwenda kufanyika nchini Morocco," amesema

Aidha, Mwamposa amempongeza  Makonda kwa kipawa na neema kubwa aliyonayo katika dhamira yake njema ya kustawisha maisha na ndoto za vijana wengi wa kitanzania.

Mwamposa amemtaka Makonda kuendelea kushughulika na ustawi wa wananchi anaowaongoza.

"Wote mnakubaliana kuwa Rais wetu kumteua Mheshimiwa Paul Makonda kwamba Mungu alimuongoza kumleta Arusha.Makonda tumefahamiana tangu akiwa chuoni na kazi hizi anazozifanya sasa sio kwa bahati, Mungu amempa hicho kipawa na Mungu amempa hiyo Neema, Mungu amempa ufahamu wa kufanya mambo makubwa tangu nimemfahamu", Amesema  Mwamposa.