BENKI ya Dunia (WB) imemchagua Dk. Zarau Kibwe, raia wa Tanzania, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi 22 ikiwamo Tanzania.
Dk. Kibwe anakuwa Mtanzania wa pili kushika nafasi hiyo kutoka Tanzania. Mtanzania wa kwanza kuhudumu katika nafasi hiyo alikuwa Christopher Kahag, mwaka 1968 hadi 1970.
Uteuzi wa Dk. Kibwe katika nafasi hiyo nyeti kwenye taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani, umetangazwa katika Mkutano wa Mwaka wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Benki ya Dunia, uliofanyika jijini Washington D.C, Marekani ambako Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha Duniani IMF na Benki ya Dunia inafanyika.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo, Dk. Kibwe alihudumu katika Ofisi hiyo ya Bodi kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Mshauri na Mshauri Mwandamizi kwa zaidi ya miaka saba, tangu mwaka 2017.
Akizungumza jijini Washington D.C, baada ya kutangazwa kuchukua nafasi hiyo, Dk. Kibwe alisema ataitumia nafasi hiyo kusimamia uendeshaji wa benki na taasisi zake pamoja na kutetea maslahi ya nchi katika Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia na maslahi ya Kanda ya Afrika anayoisimamia ili kukuza maendeleo na uchumi wa nchi hizo.
Akizungumza kwa niaba ya serikali katika mkutano huo uliomtangaza Dk. Kibwe kuchukua nafasi hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika mikutano hiyo ya mwaka ya IMF na Benki ya Dunia, alisema hayo ni matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, kuifungua nchi na kukuza diplomasia ya kimataifa.
Dk. Nchemba alimpongeza Dk. Kibwe kwa kupata nafasi hiyo na kwamba kutokana na umahili wake katika masuala ya uchumi na fedha, pamoja na uzoefu wake wa muda mrefu katika ofisi hiyo, anaamini kuwa maslahi ya nchi yataendelea kulindwa ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania.
Dk. Kibwe ni mchumi na kwa nafasi hiyo atakuwa mkurugenzi mtendaji wa kanda inayojumuisha nchi za Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Shelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.
Kabla ya kujiunga na Ofisi ya Bodi, Dk. Kibwe alihudumu kama Mchumi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania. Katika kipindi cha miaka 15 ya kazi yake, Dk. Kibwe alihudumu katika Serikali ya Jamhuri wa Muungano katika nafasi mbalimbali ikiwamo ya Mchambuzi Mwandamizi wa Sera katika Ofisi ya Rais – Tume ya Mipango, Mhadhiri Msaidizi (Chuo Kikuu Dodoma), Ofisa Forodha Msaidizi (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na Mhadhiri Msaidizi Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Dk. Kibwe ana Shahada ya Uzamivu (Ph.D.) katika Uchumi wa Maendeleo, Shahada ya Uzamili (MA) katika Uchumi wa Maendeleo na Shahada ya Umahiri katika Sera za Umma, zote kutoka Taasisi ya Taifa ya Mafunzo ya Sera (GRIPS) Tokyo, Japan.
Alipata Shahada ya Kwanza ya Sayansi katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe kilichoko Morogoro, Tanzania.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED