Mtaalam aanika mbinu kukabili mafuriko

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 01:30 PM Apr 25 2024
Mtaalam wa mabadiliko tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Pius Yanda
PICHA: MAKTABA
Mtaalam wa mabadiliko tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Pius Yanda

MTAALAM wa mabadiliko tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Pius Yanda, ameishauri serikali kupanua mitaro ya barabarani iwe na uwezo wa kusafirisha maji yanayotiririka kwa kiasi kikubwa ili kuepuka mafuriko yanayojitokeza na kuathiri wananchi.

Pia ametoa ushauri huo wakati maeneo mengi nchini hasa mikoa ya Kanda ya Pwani, yaani Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara kukumbwa na mvua kubwa iliyosababisha maafa kwa binadamu na uharibifu wa miundombinu huku zaidi ya watu 60 wakifariki dunia.Amewakati mitaro hiyo inajengwa kasi ya mvua haikuwa kubwa, hivyo kuna haja ya kuipanua ili kuhimili kubeba maji yanayoendana na kiwango cha mvua kinachonyesha sasa.

"Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mvua si nyingi zinanyesha kwa muda mfupi, lakini zinanyesha kwa kiwango kikubwa na kusababisha mitaro kuzidiwa hivyo kunatokea mafuriko kama tunayoyashuhudia sasa," amesema. 

Prof. Yanda ameliishauri pia serikali kupitia idara za mipango miji katika halmashauri kuanza kufikiria kujenga majengo yanayofaa kulingana na jiografia ya eneo husika, ili kuwapo na nafasi ya kutosha kupisha mkondo wa asili wa maji kupita na kuepuka mafuriko.

Amesema  tatizo la mafuriko pia linachangiwa na wananchi kujenga katika maeneo ambayo ni mkondo wa asili wa maji hivyo mvua zinaponyesha yanakosa njia ya kupita na kuishia kujaa barabarani na kwenye makazi ya watu.

Pia ametaja maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo hupelekea watu kujenga nyumba za kisasa zilizosakafiwa na kuwekwa 'tiles' hivyo maji hukusanywa juu ya sakafu badala ya kunyonywa ardhini kama ilivyokuwa hapo awali.

Mtaalamu huyo wa mazingira pia ametaja usimamizi usiojitosheleza  wa taka ngumu kusababisha kuzagaa mitaani na kuishia kwenye mitaro ambayo huziba na kushindwa kupeleka maji maeneo yanayofaa na kushauri manispaa kulisimamia ipasavyo suala hilo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga, amesema ili kumaliza tatizo hilo kunahitaji juhudi za pamoja za taasisi husika kama vile Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Manispaa zote.

Amesema kwa upande wao, wanapunguza madhara kwa kusafisha  na kuzibua mitaro iliyopo barabarani ingawa mitaro hiyo inazidiwa kwa kuwa maji yanakosa njia za kupita baada ya mkondo wake kuzibwa na makazi ya watu.

Ameshauri pia manispaa kusimamia zoezi la ugawaji wa viwanja ili kuhakikisha wananchi hawajengi maeneo ambayo ni mikondo ya asili ya maji kwa kuwa ni moja ya sababu za mafuriko.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Manispaa ya Kinondoni, Aquilinus Shinduki, amesema kama manispaa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kuwa wanasimamia taka zisimwagwe kwenye mitaro hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa jamii.

"Kwa mfano sisi Manispaa ya Kinondoni tumetenga fungu kwa ajili ya kuzibua mitaro katika eneo letu, na ni suala ambalo ni endelevu kwa hiyo tunaamini kadiri siku zinavyoendelea tutapunguza adha hii kwa kiasi kikubwa" amesema.

Amesema pia Idara ya Mipangomiji inaendelea kusimamia na kuzuia ujenzi wa holela hasa kwenye  kuwahamasisha wananchi waliojenga kwenye mabonde na pembezoni mwa mito kuhama ili maji yapite kwa uhuru na kuepusha mafuriko yanayoleta maafa kwa jamii.

TAARIFA TMA 

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa angalizo la kuendelea kuwapo na mvua kubwa kwa baadhi ya mikoa nchini ikiwamo Dar es Salaam, Tanga na Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba mpaka kesho.

Katika angalizo la kuwapo upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika  mita mbili kwa baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi.

Mamlaka hiyo imeeleza kuna uwezekano wa kutokea athari ikiwamo vifo, uharibifu wa miundombinu, nyumba kujaa maji na watu kukosa makazi na kuwaelekeza watu kuchukua tahadhari.