Msipeleke wenye selimundu kwa waganga wa kienyeji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:45 AM Sep 15 2024
sickle cells
Picha: Mtandao
sickle cells

KUTOKANA na kukosekana kwa elimu ya ugonjwa wa selimundu ( sickle cells) nchini,baadhi ya wazazi wa watoto wenye ugonjwa huom,wanadaiwa kuwa na imani potofu na kuishia kupeleka watoto wao kwa waganga wa kienyeji badala ya kuwapeleka hospitali.

Kutokana na hilo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya nchini wameombwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huo na kuongeza uelewa ili kuepusha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vitokanavyo na kukosa matibabu.

Hayo yamesemwa jana jijini Arusha na  mwanaharakati na shujaa wa  selimundu, anayepambana kuelewesha juu ya ugonjwa huo, Sanyu Senga, akizungumza na wadau katika kampeni ya kuelimisha jamii.

Ametaja changamoto kubwa hapa nchini ya ugonjwa huo kutokuwa na sauti,hali inayosababisha imani potofu kwa baadhi ya wazazi.

“Baadhi ya wazazi wakigundua watoto wao wana selimundu wanaenda kwa waganga wa kienyeji,hawaji hospitali na wengine wakiwapeleka kwenye maombi na ksuahau kuwa Mungu ana nafasi yake ila ushauri wa kitaalamu una nafasi kubwa zaidi,”

“Tuna wajibu wa kuhamasisha jamii zaidi ili wanapobaini watoto wao wana ugonjwa huo wawapeleke hospitali, mimi ni shujaa wa ugonjwa huu na nina umri wa miaka 47,nina mtoto na haya yote yamewezekana kwa sababu nimepata elimu,”amesema

Sanyu amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa makundi mbalimbali ambapo mwezi Septemba hutumika kwa ajili ya kuhamasisha jamii.

“Huu ni ugonjwa wa kurithi ambao tunapata kwa wazazi wote wawili,tunaelimisha wanaotaka kuanzisha familia wapime kujua vinasaba vyao kama ambavyo tumekuwa na utaratibu wa kupima Virusi vya Ukimwi,tufanye hivi  kwenye selimundu hiyo ndiyo vunja mduara,”amesema

Awali mwanzilishi wa Taasisi ya Sickle cell Disease Patients Community of Tanzania, Arafa Said, amesema lengo ni kuhakikisha wanaongeza uelewa kwa jamii na matibabu bora kwa wenye ugonjwa huo.

“Sisi tunajua changamoto ambayo tunapitia naamini huwezi kuvaa kiatu ambacho hakikutoshi,tuko hapa kuadhimishamwezi huu wa kuongeza uelewa katika jamii na wadau wameamua kutupa ushirikiano na watapanda Mlima ilimanajro kwa niaba ya wagonjwa ili kufikisha ujumbe,”amesema

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Sickle Forward, nchini Marekani, Dk  Allan Anderson, ambaye ameongozana na wanaharakati wengine zaidi ya 20, watapanda Mlima Kilimanjaro,kwa lengo la kukusanya fedha zitakazotolewa kwa ajili ya watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huo katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Tunalenga kuongeza utambuzi wa haraka wa watoto wachanga ili kuanza matibabu mapema katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara,tuko kwenye mwezi huu wa uhamasishaji na tunashirikiana na serikali na wadau wengine,”amesema Dk Allan

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa wanajua umuhimu wa kusaidia vitendanishi kwa ajili ya kupima ugonjwa huo kwani itasaidia kuokoa vifo vya watoto wadogo vitokanavyo na ugonjwa huo ambapo hadi sasa wameshakusanya zaidi ya Dola za Marekani1.2 milioni kwa ajili ya kusaidia nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Lengo letu ni kusaidia uchunguzi na matibabu katika maeneo ya nchi hizo,pamoja na nyingine na tunafanya kazi nan chi za Afrika Magharibi pia ikiwemo Mali, Togo,Gabon,”ameongeza

Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Arusha, Dk Edna Ntulwe, amesema kwa mwaka hapa nchini watoto zaidi ya 10,000 hugundulika kuwa na ugonjwa huo na kuwa ni muhimu elimu kuendelea kutolewa ili kukata mnyororo wa kuzaliwa watoto wenye selimundu.

Mtendaji Mkuu wa asasi ya mwamvuli ya wadau wanaofanya kazi kwenye ugonjwa huo (Tanzania Sickle Cell Disease Alliance), Dk Deogratias Matanda,amesema tatizo la selimundu nchini bado ni kubwa nchini.

“Kati ya watoto zaidi ya 10,000 wanaozaliwa na tatizo hilo kati yao tusipotambua mapema na kuanza matibabu,asilimia 70 hadi 90 hufariki kabla ya kufika umri wa miaka mtano,”amesema