MKURUGENZI wa Kampuni ya Atlantic Micro Credit Ltd, Wendy Ishengoma (38) na wenzake watatu wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuendesha biashara ya upatu kinyume na sheria na kutakatisha fedha Sh. bilioni 3.9.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sultan Mdee (29) Mhasibu Mkazi wa Goba, Frank Tengia (34), Meneja wa Tawi hilo, mkazi wa Mbezi Juu na Mwiga Mwiga (31), Ofisa Masoko.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Neema Moshi, akisaidiana na Judith Kyamba, alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa washtakiwa wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwamo la kuongoza genge la uhalifu.
Kyamba alidai kuwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanatuhumiwa Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 wakiwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa makusudi waliongoza na kusimamia genge la uhalifu.
Katika shtaka la pili, washtakiwa watuhumiwa tarehe hiyo na eneo hilo wanatuhumiwa kusimamia mpango wa piramidi kwa kutoa ahadi kwa wanachama waliotajwa kwenye mikataba ya ubia ya Tanzania wa Sh. 3,631,761,863 kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la utakatishaji fedha washtakiwa wanatuhumiwa kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 jijini Dar es Salaam walijipatia Sh. bilioni 3.6 wakati wakijua wanapokea fedha hizo ni mazalia ya kosa la jinai ya kuendesha biashara ya upatu kinyume na sheria.
Wakili Moshi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mashtaka yanayowakabili, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza na pia hayana dhamana kisheria.
Kesi imeahirishwa hadi Novemba 11, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED