Wanaharakati sheria, wacharuka na marekebisho haki ya mama msibani

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:32 AM Nov 29 2024
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Picha: Mtandao
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.

KATIKA Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati wa kupinga ukatili huo wa kijinsia ikiwa ni kuelekea miaka 30+ ya Beijing mwaka kesho, Mtandao wa Kupinga Ukatili Tanzania (MKUKI), umebainisha mambo mengi yanayopaswa kufanyiwa kazi kukomesha vitendo hivyo, ikiwamo sheria za ardhi.

MKUKI wanasema, miongoni mwa yanayopaswa  kushughulikiwa ni yanayogusa moja kwa moja familia, zikiwamo Sheria ya Ardhi ya Kimila na Sheria ya Ndoa, inayotumika sana kurudisha maendeleo ya kiuchumi kwa mwanamke, ikimnyima kumiliki mali kama alivyo mwanaume kwenye familia.

Inataja hata mke anapochangia kwenye ndoa yake kupatikana ardhi au mali nyinginezo na bahati mbaya mwenza wake akitangulia mbele za haki, mwanamke amekuwa akinyang`anywa ardhi.

Wanaitaja ni pamoja na mali nyinginezo alizoshiriki kuzipata, hivyo kuanza maisha upya, akitaabika na watoto wake.

 MKUKI WALIKOIBUKIA 

Watetezi sheria wa MKUKI, anapaza sauti akiiomba serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na wizara nyinginezo za kisketa, kuliangalia hilo na kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.

Hapo kuna eneo la ardhi ya kimila na Sheria ya ndoa ili kumnusuru mwanamke na kadhia hiyo ya ukatili ambayo imekuwa ikimdidimiza na kumrudisha nyuma kiuchumi.

Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Dk. Monica Muhoja, anatamka haja ya kuongeza kasi zaidi katika kumuinua mwanamke.

Hilo linashauriwa kuendana na kutungwa sheria maalum za kupinga ukatili wa kijinsia, ambao umekuwa tatizo kubwa katika maisha ya mwanamke, hasa zile zinazogusa familia moja kwa moja.

“Kwa mfano, sheria za mirathi na Sheria ya Ndoa, zinabagua sana wanawake na mabinti hususani wajane. Hizi zinachangia wengi kurudi nyuma kiuchumi na kupata matatizo ya afya ya akili kwa sababu wanakuwa wanakandamizwa sana,” anasema. 

Dk. Monica anaendelea: “Kwa hiyo tuko pamoja na serikali kushirikiana kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa.”

haki ardhi.jpg 76.39 KB

 Anasema, tayari wamebainisha maeneo wanayotamani yafanyiwe kazi na kwamba, wako tayari kukaa na serikali kushirikiana kuyachambua kwa pamoja na kuona namna mbavyo wanaweza kutatua hilo.

"Mwaka huu tumekuja na maombi mengine ambapo tunaomba serikali kuyashughulia ikiwamo kulifikisha jambo hili kwenye agenda za kiusalama kwa kuhakikisha kuwa masuala ya ukatili wa kijinsia, yanaingizwa rasmi katika mipango na mikakati ya kiusalama ya kitaifa.

"Maombi mengine, ni pamoja na kuomba kutungwa kwa sheria mahsusi ambayo italinda jamii hasa wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili huo wa kijinsia,” anasema.

KUTOKA UBALOZINI

Balozi wa Umoja wa Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya nchini, Christine Grau, anasema ukatili wa kijinsia ni tatizo la dunia na limekuwa likiathiri zaidi wanawake na watoto hivyo ni lazima kila mmoja apambane kulitokomeza.

 "Tunaweza kuchagua kuiwezesha jamii kuzuia hili na namna ya kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya unyanyasaji huo wa kijinsia, kuripoti kesi na kutoa huduma bora kwa waathirika ikiwa ni pamoja na wale waliotengwa zaidi na walio hatarini,”anasema Balozi Christine.

 Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan, anasema kukomesha ukatili wa kijinsia inawezekana endapo kila mmoja atakubali kushiriki katika mapambano hayo ikiwamo kukataa kuozesha wasichana katika umri mdogo kabla ya kutimiza miaka 18.

 Mratibu Mkazi wa Umoa wa Mataifa Tanzania, Suzan Namondo, anasema: “Tunapokaribia kuadhimisha Miaka 30 ya Beijing, tuna nafasi ya kutafakari namna ya kukabiliana na changamoto hiyo inayoendelea ya ukatili wa kijinsia na kupanga mbinu za dhati za kulitokomeza.”

 Anna Kulaya, Mkurugenzi wa WiLDAF, anasema dhamira ya kampeni hiyo ni kushawishi na kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo inayochochea unyanyasaji na ukandamizaji kijinsia, kukuza usawa, heshima na haki kwa wote.

 “Leo ni siku muhimu sana kwetu sote tunapoanza safari ya kuelekea Siku 16 za Uanaharakati wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia. 

“Hii ni fursa ya kipekee ya kushirikiana, kuhamasisha na kuchukua hatua za pamoja dhidi ya aina zote za ukatili wa kijinsia kwa ajili ya jamii yenye usawa, heshima na haki na maendeleo kwa wote.

“Muungano huu ulipoanzishwa ulikuwa na mashirika tisa tu, lakini kwa miaka kadhaa umeendelea kukua na kuvutia wanachama wengi, kutokana na juhudi zake za pamoja za kupinga ukatili wa kijinsia na kukuza usawa wa kijinsia katika jamii, lengo kubwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki katika nchi iliyo huru,” anasema Kulaya. 

 Kulaya anaendelea; “Mkuki ni muungano mkubwa wa mashirika zaidi ya 200, unaofanya kazi chini ya uratibu wa WiLDAF ambayo dhamira yake kuu ni kushawishi na kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo inayochochea unyanyasaji na ukandamizaji wa kijinsia, huku ikikuza usawa, heshima na haki kwa wote. 

 "Kupitia kampeni hii, MKUKI  inalenga kuwa sauti ya mabadiliko na chachu ya jamii yenye amani, heshima, na utu kwa kila mtu bila kujali jinsia,"anasema. 

WAZIRI SHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema serikali ipo tayari kuyapokea maombi hayo na kukaa kwa pamoja na wadau hao kuyajadili  ili kuona namna gani hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa.

Anasema suala la ukatili wa kijinsia ni la aibu linalobeza kundi kubwa katika jamii na si la kifahari kulitetea na kwamba  linalohitaji kutokomezwa kwa kuchukua hatua stahiki.

 Prof. Kabudi anasema licha ya Tanzania kupiga hatua katika mapambano katika eneo hilo, bado nguvu kubwa inahitajika kupiga hatua zaidi na kutaka kila mmoja awe balozi wa kupinga ukatili huo wa kijinsia.

“Kama ambavyo kaulimbiu ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wakijinsia inayosema Kuelekea ‘Miaka 30+ ya Beijing’, chagua kutokomeza ukatili’ hii iwakumbushe watu wote kujitafakari na kujitathimini yale yanayofanywa kama yanatija,” anasema Prof.Kabudi.

“Jambo hili halipaswi kuvumiliwa kabisa, hivyo niombe kila mmoja wetu tuendeleze mapambano ni ukatili, kazi hii iwe endelevu, isiishie kwenye hizi iku 16 na sisi kama serikali tutaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia na kulinda utu wa mwanamke katika maeneo yote.”