KIKOSI cha Yanga jana mchana kiliwasili mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo unaotarajiwa kuchezwa kesho, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sead Ramovic, akiahidi kurejea kwa kasi ligi kuu baada ya kurekebisha mapungufu aliyoyaona kwenye mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan uliochezwa Jumanne iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga imewasili Lindi ikiwa na kikosi kamili tayari kuwafuta machozi mashabiki wake ambao wamekosa furaha baada ya kupata vichapo vitatu mfululizo katika mechi tatu zilizopita.
Yanga walianza kufungwa kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Azam FC walipofungwa bao 1-0 na baadae kupata kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Tabora United kabla ya jumanne iliyopita kufungwa mabao 2-0 na Al Hilal.
Akizungumza jana muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuifuata Namungo, Ramovic amesema kwa sasa wamefanyia kazi mapungufu aliyoyaona kwenye mchezo uliopita dhidi ya Al Hilal na sasa wapo tayari kwa mchezo huo wa kesho.
"Kama nilivyosema suala ya utimamu huwezi kulitatua kwa muda mfupi, lakini tumeanza kulifanyia kazi, na nadhani linaweza kukaa sawa baada ya muda, kwa sasa nataka turejee kwenye michezo ya Ligi kwa kasi" alisema Ramovic.
Mchezo huo wa leo, utakuwa wa kwanza kwa kocha huyo kuiongoza Yanga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kuondoka kwa Miguel Gamondi ambaye aliipa ubingwa msimu uliopita na msimu huu aliiongoza kwenye michezo 10, ikishinda minane na kupoteza miwili.
Mara baada ya mechi dhidi ya Al Hilal, Ramovic alibainisha kuwa wachezaji wake walionekana hawana utimamu wa mwili pamoja na pumzi ya kucheza kwa dakika 90 kwa nguvu ile ile, hivyo kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, aliwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kusahau yaliyopita na kuganga yajayo akiwataka kujitokeza kwa wingi ili kuipa sapoti timu yao.
"Malengo yetu kwa sasa ni mchezo wa Jumamosi dhidi ya Namungo, ushindi ni muhimu sana kwenye mechi hii ili kupunguza pengo la pointi na anayeongoza.
Tunajua muda ni mdogo sana kutoka mechi iliyopita hadi hii, lakini tumejiandaa kupambana na mashabiki wanatakiwa kwenda kuipambania timu yao," alisema Kamwe.
Alikiri kuwa ni kweli wanapitia kipindi kigumu, lakini bado hawana msimu mbaya kwani wamezidiwa pointi nne tu na wapinzani wao na kama wakipata ushindi na kufanana michezo, itasalia pointi moja tu.
Yanga inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu mpaka sasa ikiwa na pointi 24, sawa na Azam FC yenye pointi 24, lakini wanalambalamba wameruhusu mabao matatu, Wanajangwani wakiruhusu mabao manne.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED