WATU watatu wamefariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa , katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Mbembela, Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, ajali hiyo ilitokea Novemba 27, 2024 majira ya saa 12 jioni, kwenye barabara kuu ya Mbeya-Tunduma.
Kamanda Kuzaga amesema lori namba T.537 DNC aina ya FAW, lililokuwa na tela namba T.241 ARG, likitokea Dar es Salaam kuelekea Tunduma mkoani Songwe, likiwa limebeba madini ya Sulphur, lilipoteza uelekeo na kugonga magari sita, bajaji nne, na pikipiki moja.
Ameyataja magari yaliyohusika katika ajali hiyo ni T.199 DYF Toyota Coaster, SU 44682 Toyota Double Cabin mali ya Shirika la Posta Mbeya iliyokuwa ikiendeshwa na Fredy Mwasanga (48), mkazi wa Soweto, gari T.134 DXK Toyota Double Cabin, iliyokuwa ikiendeshwa na Lusekelo Mwaseba (48) mkazi wa Sae, Gari T.370 ABN Toyota Land Cruiser, gari T.344 BTS Toyota Cresta na gari T.474 EHL/t.449 EHL aina ya FAW iliyokuwa ikiendeshwa na Alon Ruben (50) mkazi wa Isanga.
“Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu watatu, wawili wakiwa wanaume na mmoja wa kike, na majeruhi tisa wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya,” amesema Kamanda Kuzaga.
Amebainisha chanzo cha ajali hiyuo kuwa ni uzembe wa dereva ambaye alishindwa kulimudu gari katika eneo lenye mteremko na alikimbia, amesema jitihada za kumtafuta dereva zinaendelea kwa kushirikiana na mmiliki wa gari.
Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED