MNAMO Februari mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, ametamka kuwa Sekta ya Viwanda, pia Utalii na Madini, zimevunja rekodi kuingiza mapato makubwa zaidi tangu Tanzania ipate uhuru.
Pia, mwezi Agosti mwaka huu akazungumzia mapinduzi viwanda mkoani Morogoro, akitamka bayana kwamba serikali iko tayari kubadilisha sera na sheria za nchi, ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, lengo kujihakikishia uzalishaji chakula cha kutosha kwa mahitaji ya ndani na nje.
Katika ufafanuzi wake, Rais Dk. Samia akasema serikali itaendelea kuwapa wakulima ruzuku ya mbolea na inajipanga kuwapa ruzuku za mbegu, ili kupunguza changamoto za uzalishaji mazao, wakulima wafurahie matunda ya kazi zao.
Baada ya Rais kuingia madarakani Machi 2021, mabadiliko makubwa yameanza kuonekana kwenye uchumi, mauzo ya nje ya bidhaa nchini, yameongezeka na kuvuka Dola za Marekani bilioni saba (shilingi trilioni 18) kwa mwaka kwa mara ya kwanza.
Hiyo inatajwa kuvuka Dola za Marekani bilioni saba kwa miaka miwili mfululizo; mwaka 2022 na 2023.
USHUHUDA WA MORO
Katika kuliunga mkono hilo, mkoa wa Morogoro umejiwekea mipango ya kuwa na mazao ya kimkakati kukuza uchumi wa wakulima na nchi.
Hiyo inajumuisha kuwekeza ili kurejesha historia viwanda, wakianza na vya mazao ya viungo vya chakula vikubwa vitatu, vya kati 10 na vidogo 50 vinavyotarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Katibu Tawala wa Mkoa Dk. Musa Ally Musa, anasema mazao hayo ya viungo yana nafasi kubwa kuleta tija katika uchumi wa mkoa.
Anataja kilimo chenye tija Morogoro, mikakati yake ipo katika hatua mbalimbali za kuhimiza mazao hayo tajwa, kwa mwaka 2022 hadi 2025.
Vilevile, Katibu Tawala, anasema mwaka 2026 hadi 2028 wanahihimiza uanzishwaji viwanda na sasa mkoa una kiwanda kimoja cha viungo vya chakula viwanda vingine vidogo vitatu.
Pia, Dk. Musa anasema kuna viwanda vingine vidogo 50 vinavyoundwa na vikundi vya wanawake na vijana, ambao pia ni wakulima na wazalishaji wadogo wa bidhaa za viungo.
Rai yake, wakati umefika wakulima wakajikita kuzalisha viungo vya chakula, ili kuendana na mahitaji ya tani zaidi ya 100 kila mwaka kwa soko la ndani na nje ya nchi. Mpaka sasa inapatikana tani 30, sawa na asilimia 30.
Katibu Tawala anasema, mbali na karafuu, katika mazao viungo mengine ni; mchaichai, mdalasini, hiriki, karafuu, tangawizi, binzari, vanila, pilipili manga, vitunguu saumu na kakao yanayolimwa mkoani Morogoro.
Anasema ina masoko makubwa ndani na nje ya nchi, Morogoro inatoa tani 2000 za karafuu, sawaa na nusu zinazozalishwa Zanzibar kwa mwaka, ikikisiwa baada ya miaka mitano ijayo, Morogoro itaivuka tani 4000 za Zanzibar.
UMAARUFU WA KARAFUU
Kwa mujibu wa Dk. Musa, masoko yako dunia nzima yakiwamo nchini Uingereza, Canada na Ujerumani, anaitaja karafuu ina wateja wengiwanaitumia kwenye viungo vya chakula, dawa za meno, sabuni na hata sigara.
Dk. Musa anasema mkarafuu ukipandwa unahifadhi misitu na hauathiri mazingira, hivyo anawataka wakulima kuondoa hofu ya kilmo cha muda mrefu na kipato cha kila siku, kwa sababu inaweza kulimwa na mazao mengine ya muda mfupi katika eneo moja.
UWEKEZAJI ULIVYO
Uwekezaji kimkoa, Dk. Musa anasema serikali imeshajenga maghala matatu wilayani Morogoro, kuwasaidia wakulima kuhifadhi mazao yao, sambamba na kuuza na kupata malipo kupitia taasisi za kifedha, wakiondokana wizi, pia upokeaji pesa bandia.
“Suala la kulipwa fedha kupitia benki, linamsaidia mkulima kupata pesa nyingi, tofauti na kuuza kupitia rejareja inayomfanya mkulima kushawishika na kujiingiza kwenye mikopo,” anasema na kuendelea:
Anafafanua, tayari mkoa umeshaunda Ushirika wa Kilimo cha Karafuu kwa kata nane za wilaya ya Morogoro, ili kuwawezesha kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha, zikiwamo benki kadhaa, waendeleze kilimo kwa manufaa yao na taifa
Anasema, bei ya karafuu ya Morogoro, katika soko la Dar es Salaam, inauzwa shilingi 28,000 kwa kilo moja dukani na mkoani Morogoro ni shilingi 23,000, akiitetea sokoni hapo karafuu ni mali.
Dk. Musa anatumia mfano, wastani wa karafuu ingeuzwa shilingi 20,000 kwa kilo, wakulima wangeingiza shilingi bilioni 40 kwa mkoa na halmashauri husika zingepata shilingi bilioni 1.8 kwa zao karafuu.
Hapo anafafanua, kila ekari inachukua mimea ya karafuu 40 hadi 45 na inakisiwa ikizaa vizuri mkulima hakosi shilingi milioni kati ya tisa na 13 kwa mwaka.
“Familia moja yenye watu wanne hadi sita ina uwezo wa kupata (shilingi) milioni tisa hadi 3 kwa mwaka na hapo mkulima ana uwezo wa kutumia shilingi milioni moja kwa mwezi au laki nane kwa mwezi. Sasa kilimo hicho si ni sawa na mshahara wa mtu mwenye digirii?!” Anatoa tathmini Katibu Tawala huyo.
CHANGAMOTO INAVYOKABILIWA
Dk. Musa anasema, Morogoro kupitia mauzo ghalani, inajipanga kukabiliana na changamoto za wakulima hao wa viungo.
Anataja makonyo ambayo yangeweza kumuingiza fedha, lakini wachuuzi ‘huwalalia’ wakulima wakinunua klwa bei ya shilingi 500 badala ya 1,500 kwa kilo, kama ilivyo kwa wenzao wa Zanzibar.
Anasema kuwapo elimu ndogo ya karafuu, mkoa umeshawapeleka Zanzibar wakulima zaidi ya 50 kujifunza namna ya kuandaa shamba lake, hadi mavuno.
Katibu Tawala anafafanua kuwapo mapungufi ya usimamizi wa mashamba ya mikatafuu umewafanya baadhi ya wakulima kushindwa kuvuna inavyotakiwa.
Aidha, anasema wamejipanga kukabiliana na kushuka uzalishaji, wakitenga kundi la vijana wanaopatiwa vifaa na miche wapande kwenye vitalu na kuwauzia wataalamu kilimo kwenye ofisi ya mkoa na halmashauri kwa bei shilingi 1000 kila mche.
Dk. Musa anasema tangu mwaka 2022 kampeni ya kilimo cha mkarafuu ilipoanza, tayari miche 500,000 imeshagaiwa bure kwa wakulima na mkoa unatarajia kugawa miche milioni moja hadi kufika mwishoni wa mwaka huu.
Anataja baadhi ya maeneo ya mkoa yanakolimwa mazao hayo ni wilaya za: Morogoro, Gairo kwenye milima ya Nongwe, Mvomero - Turiani na Kilosa.
Dk. Musa anaiomba Wizara ya Kilimo kuwekeza kwenye mazao ya viungo na kusaidia utafiti na pembejeo, ili kufanya mazao hayo yawe rafiki kwa mazingira yao na kuleta tija shamabani.
Hata hivyo, annakiri Wizara ya Kilimo imejitahidi kuingalia sekta ya kilimo katika nyanja zingine.
MAKATIBU TAWALA MSAIDIZI
Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mali Dk. Rosalia Rwegasira, anasema Morogoro ina malengo ya kuzalisha miche milioni mbili ya karafuu na kakao milioni 2.5, itakayosaimbazwa kwa wananchi.
Naye Katibu Tawala Msadizi (Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Beatrice Njawa, anawataja mahsusi wanawake na vijana, kwa sasa wamejikita kuzalishaji mazao hayo ya viungo vya chakula, ingawa kuna changamoto ya kukosa nembo ya kudhibiti ubora (TBS).
Njawa anasema kuanzishwa viwanda Morogoro, kutawasaidia wakulima na wazalishaji bidhaa hizo, wakipata nembo za kufanya biashara ndani na nje ya nchi kwa maslahi yao na nchi.
KUTOKA KIWANDANI
Meneja uzalishaji wa kampuni inayojishughulika na kukausha mazao ya viungo Abel Gaima, anawataka wakulima kuongeza nguvu katika kilimo, kwani bado wanapata theluthi ya malighafu kutoka kwa wakulima, yaani tani 30, huku kunaa hitaji la tani 100 kwa mwaka.
Pia, anasema bei za bidhaa ya karafuu ni kubwa, tofauti na bidhaa nyingine, akitoa mfano kilo moja ni shilingi 19,500 kwa kilo.
Ofisa Usalama wa Chakula anayehusika na ukausha hiriki, Heavenlight Riziki, anaishukuru serikali mkoani kuhimiza jamii kujikita kwenye kilimo cha mazao viungo, akiamini inasaidia upatikanaji bidhaa hizo adimu, licha ya uhitaji mkubwa.
Hapo anaungwa mkono na mtuimishi wa kampuni hiyo, mkuloim wa karafuu kutoka Kata ya Kibogwa Tarafa ya Matombo, Morogoro, Omari Saidi, anayeiomba serikali kuimarisha maghala ya wazi ya karafuu, kwa ufanisi wa tija ya uzalishaji na manufaa ya malipo yao.
Pia, anaiomba serikali ikaboresha miundombinu ya barabara na madaraja, kuwaepushia wakulima changamoto za uusafirishaji bidhaa zao, kutoka shambani hadi sokoni, pia kunufaisha wanunuzi wa bidhaa zao.
Pia, wakulima wanaiambia Nipashe, wanakabiliwa na ukosefu wa mashine ya kukatishia ushuru, hali inayofanya mapato ya mazao yao kutoingia kwenye baadhi ya Kata kama Matombo na kwenda kata jirani ya Kinole.
Taarifa ya Kilimo Mkoa, Morogoro ina eneo la hekta 2,226,396 linalofaa kwa Kilimo, lakii linalolimwa sasa ni wastani wa hekta 960,034 sawa na asilimia 43.
Pia, eneo linalofaa kwa Kilimo cha Umwagiliaji ni hekta 1,510,339.51 na eneo linalomwagiliwa kwa sasa ni wastani wa hekta 79,429 sawa na asilimia 5 ambapo Mkoa una Skimu za Umwagiliaji 106 (asili na zilizoendelezwa) zinazotambulika zenye ukubwa wa hekta 323,758.15.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, akasema licha ya biashara ndogo na za kati nchini kutoa ajira nyingi, inavochangia pato la taifa, kundi hilo la wazalishaji linakabiliwa na changamoto kama za masoko na kukosa mikopo.
Anasema, hivi sasa serikali iko mbioni kupitia Sera ya Uanzishwa Viwanda, Sera ya Taifa, Uwekezaji ya Mwaka 1996; Sera ya Maendeleo ya Viwanda (1996-. 2020) na Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (2003), ili ziendane na mazingira ya sasa, kukidhi mahitaji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED