WAZIRI wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda, ametahadharisha kuwa kuna hatari kubwa teknolojia ikawaleta makanjanja wengi kwenye tasnia ya habari ambao hawana elimu na masuala ya habari kama hatua hazitachukuliwa haraka.
Amesema makanjanja hao wataonekana wao ndio wasemaji wa habari za propaganda ambazo zitawatenganisha waandishi wa habari na serikali na kusababisha mafarakano, wataondoa mshikamano kwa nchi na hivyo tasnia ya habari kupoteza nia kama mhimili wa nne usio rasmi.
Prof. Mkenda alisema hayo juzi wakati wa mkutano mkuu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) unaofanyika mjini Singida na kuwashirikisha wenyeviti, makatibu na waweka hazina kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
"Teknolojia ya sasa hivi inasababisha habari tunazozipata hazitoki tu kwenye media (vyombo vya habari) ambazo tumezizoea, wapo watu wanajikalia wanaanzisha utangazaji na kuanza kusambaza habari, hawa nao wana nguvu ya kujenga au kubomoa.
"Kama Wizara ya Elimu tungepata mawazo yenu, tunaendelea kuelimishana waandishi wa habari kwa namna gani, mambo yapi mapya tuyaingize kwenye mitaala yetu, ni nini tufanye hata baada ya mtu kuhitimu kwa ajili ya kuendelea kujengeana uwezo," alisema.
Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo, alizitaka klabu za waandishi wa habari nchini kufanya kazi kwa kuzingatia mpango mkakati wa 2023-2025 unaotekelezwa na UTPC ili kuendelea kuwavutia wafadhili kusaidia taasisi hiyo badala ya kuendekeza migogoro.
Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya, alisema klabu zinatakiwa kutimiza wajibu kwa kuwa zisipofanya hivyo, UTPC itaonekana kuwa kikwazo cha yale ambayo yangeweza kupatikana kupitia umoja huo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED