Misaada waathirika mafuriko Rufiji yazua jambo, DC ajibu

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 01:11 PM Apr 25 2024
Mkuu wa Wilaya ya Rufuji, Meja Edward Gowele.
PICHA: MAKTABA
Mkuu wa Wilaya ya Rufuji, Meja Edward Gowele.

BAADHI ya waathirika wa mafuriko katika vijiji vilivyoko kata ya Muhoro, Rufiji mkoani Pwani, wamelalamikia utaratibu wa utoaji wa misaada ya chakula iliyopelekwa na serikali na wadau mbalimbali.

Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Rufuji, Meja Edward Gowele, amefafanua madai hayo huku akiahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya waathirika hao walmesema utaratibu wa ugawaji wa misaada hiyo ya chakula hususani katika ngazi za vijiji waliko waathirika hao haiwafikii baadhi ya walengwa huku wengine wakidai kuwa  unafanywa kwa kujuana katika ngazi za vijiji.

Pia wamesema hata wachache wanaofikiwa, kiwango wanachopewa hakitoshelezi kulingana na ukubwa wa familia au kaya kwa sababu hata kinapogawiwa kidogo muda wa kuzirudia kaya hizo haujawekwa vizuri. 

Wamesema hatua hiyo inachangia baadhi ya familia kuishi katika wakati mgumu na  kutokuwa na uhakika wa chakula kila siku.

Jambo lingine lililobainishwa na waathirika hao ni kwamba kwa wale ambao wako katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wamekuwa wakiambiwa hawahusiki na misaada hiyo ya chakula licha ya kwamba wameathirika na mafuriko hayo.

Mohamed Seleman, mkazi wa kijiji cha Chela katika Kata ya Muhoro, amesema utaratibu wa ugawaji chakula hicho ni wa kibaguzi.

“Utaratibu wa ugawaji ni mbovu sana. Kwanza  wananchi hatushirikishwi kwamba siku gani chakula kitagawiwa. Huwa  wanashtukiza tu na ukienda unaambiwa wanagawa kwa watu wachache. Siku  moja nimeenda nikaambiwa leo ni watu 10 tu kwa hiyo nikawa nimekosa.

“Wameshagawa awamu nne lakini binafsi na familia yangu hatujabahatika hata siku moja, yaani nimepanga foleni, anapata mwenzangu mimi nakosa. Yaani wanatumia ujanja fulani hivi wa kujuana wakati wanagawa,” amesema. 

Said Mbonde, mkazi wa kijiji cha Mohoro, amesema yeye ana familia ya watu sita lakini tangu akutwe na maafa hayo, amepatiwa kiroba kidogo cha unga na mpaka sasa hajapata tena na kila akienda wanamfukuza.

“Mpaka jana (juzi), nimekwenda walipokuja lakini nikafukuzwa, wanasema  tayari mimi nilishapewa.  Sasa  hicho kiroba walichonipa kwa mara ya kwanza ndicho bado kipo mpaka sasa?” amehoji Mbonde.

Hamidu Kassim, mkazi wa kijiji cha Kipoka katika kata ya Mohoro, amesema utaratibu wa ugawaji vyakula hivyo si wa haki.

“Tunaona misaada mingi inaletwa kwa ajili ya maafa lakini tumeshuhudia utaratibu wa ugawaji kutufikia waathirika si mzuri. Hatujui  wanazingtia ukaribu, kujuana pasipo kuangalia waathirika wote kwamba wanahitaji msaada au nini.

Lakini  la kusikitisha zaidi tuna wenzetu walio kwenye mpango wa TASAF ambao nao wameathirika na wenyewe wanapokwenda kupanga foleni pale wanapotoa misaada wanafukuzwa. Wanaambiwa wao haiwahusu kwa sababu wanapatiwa na mfuko huo,” amesema Kassim. 

Fatma Sultan, amesema yeye baada ya nyumba yake kuzama na mafuriko anahifadhiwa kwenye nyumba ya jirani, hivyo anapokwenda kufuata msaada huo wa chakula amekuwa akiambiwa hastahili kwa sababu tayari amepata hifadhi.

“Nimesumbuliwa sana kila siku nikienda nafukuzwa, lakini nimekuwa sichoki kuwasumbua, kila wanapokuja huwa nakwenda kuwaambia wananiweka kwenye fungu gani kwa sababu nina hali ngumu kama waathirika wengine kwa hiyo jana (juzi), ndio nikabahatika kupewa kilo tatu za mchele na unga pamoja na maharagwe nusu wakaniambia nisirudi tena,” amesema Fatma.

Akizungumza baada ya kuwatembelea baadhi ya waathirika katika kijiji cha Muhoro, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amesema serikali inapaswa kuwagawia chakula wananchi wote walioathirika na mafuriko katika eneo hilo kwa usawa.

Akijibu malalamiko hayo baada ya kuulizwa na Nipashe, Meja Gowele amesema  endapo watabaini kuna mtendaji anagawa chakula kwa ubaguzi, atachukuliwa hatua.

“Wa kwanza wanaogawiwa ni wale walioko kwenye makambi, wa pili ni wale ambao wamepokea kaya kwenye familia zao na tatu ni watu wenye hali duni ya maisha. Ingawa  wote tumeathirika, tutachambua namna hiyo kwa kufanya tathmini ya kina,” amesema.