Katika zama hizi za uchumi wa kidijitali, simu janja imekuwa benki mfukoni. Ndani ya dakika chache, mtu anaweza kupakua programu tumizi, kujaza taarifa binafsi na kupokea mkopo bila kukanyaga ofisi yoyote ya fedha.
Kwa wengi, huu ni urahisi wa kisasa, lakini kwa baadhi ya Watanzania, mikopo ya mtandaoni imegeuka kuwa mtego wa fedheha, vitisho na msongo wa mawazo.
Mikopo hii, inayotangazwa kwa riba nafuu na masharti mepesi, imevutia maelfu ya vijana, wazazi na wafanyabiashara wadogo wanaohitaji fedha za dharura.
Hata hivyo, nyuma ya matangazo yenye mvuto, kuna simulizi za kusikitisha za kudhalilishwa, kutapeliwa na kuumizwa kisaikolojia.
Bakari John (si jina lake halisi), mkazi wa Dar es Salaam, ni miongoni mwa waliokumbwa na kadhia hiyo. Anasema alivutiwa na tangazo la taasisi moja ya mikopo mtandaoni lililoahidi kutoa Sh. 500,000 kwa masharti nafuu.
Baada ya kufuata taratibu zote za maombi, alishtuka kuona akaunti yake imeingiziwa Sh. 90,000 pekee, kiasi kisichoendana na ombi lake.
Alipowasiliana na wahudumu wa taasisi hiyo kueleza kuwa hakuhitaji kiasi hicho, alijibiwa kuwa atalazimika kulipa mkopo huo kwanza kabla ya kufanya marekebisho yoyote.
Kilichomshangaza zaidi ni ujumbe aliopokea muda mfupi baadaye. Alitakiwa kurejesha Sh 150,000 ndani ya siku sita.
"Niliwaambia sitaki mkopo huo. Niliomba ubatilishwe. Hawakujibu. Badala yake walianza kunisisitiza nilipie," anasimulia.
Alipochelewa kulipa, vitisho vilianza. Ndani ya siku chache, ndugu na marafiki zake walipokea ujumbe wa fedheha ukidai kuwa anatubu kwa kujihusisha na vitendo vya aibu na kwamba anaumwa maradhi hatari, akiomba msaada wa kulipia deni.
Ujumbe huo ulienea kwa baadhi ya watu waliokuwa kwenye orodha ya simu yake. Bakari anaamini taasisi hiyo ilipata namba hizo kupitia rukhsa ya kufikia mawasiliano yake aliyoitoa wakati wa kupakua programu.
"Nilijikuta nimevunjika moyo. Nilihisi kudhalilishwa mbele ya jamii," anasema.
Moza Ali (si jina lake halisi) wa Kibaha naye ana simulizi inayofanana. Alipakua programu ya mkopo baada ya kuvutiwa na tangazo lililoonesha kwamba akichukua Sh. 300,000 angerudisha Sh. 302,826 kwa awamu mbili, riba ndogo sana kwa mtazamo wa haraka.
Lakini baada ya kukubaliwa mkopo, masharti yakabadilika. Alielekezwa kurejesha Sh. 365,000 ndani ya mwezi mmoja, na si kwa awamu kama ilivyoahidiwa.
"Nilipowaeleza sina uwezo wa kulipa kwa mkupuo, waliniambia sikusoma vizuri masharti. Lakini tangazo lao halikuonesha hivyo," anasema.
Alipojaribu kurejesha fedha kabla ya kuzitumia, alielezwa kuwa mkopo ukishatolewa hauwezi kubatilishwa. Alipoanza kuchelewa kulipa, alipokea ujumbe wa vitisho kutoka namba tofauti zisizotambulika vizuri.
Kwa waathirika hawa, tatizo si tu riba kubwa, bali ni udhalilishaji na matumizi ya lugha ya kutisha inayolenga kumdhoofisha mkopaji kisaikolojia ili alipe haraka.
SHERIA ZINASEMAJE?
Kwa mujibu wa miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), taasisi za huduma ndogo za fedha zinapaswa kuzingatia Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha za mwaka 2019.
Kanuni hizo, hususan ibara ya 56(1)(c) na (d), zinakataza matumizi ya vitisho, nguvu au lugha ya fedheha katika ukusanyaji madeni.
Pia hairuhusiwi kuwasiliana na watu wengine wasiokuwa wadhamini wawili waliotajwa rasmi na mkopaji.
Kutuma ujumbe wa kudhalilisha kwa ndugu, marafiki au watu waliopo wenye orodha ya mawasiliano ya mkopaji ni kinyume cha sheria.
Hata hivyo, kwa mujibu wa waathirika na uchunguzi wa mwandishi wa makala hii, baadhi ya taasisi hizi zimekuwa zikikiuka wazi miongozo hiyo.
UTAPELI KIBIASHARA
Tatizo haliko kwenye mikopo pekee. Utafiti uliofanywa mwaka huu na jukwaa la biashara mtandaoni la Go7eight umebaini kuwa watu saba kati ya kumi wanaofanya biashara mtandaoni hukumbana na utapeli kwa namna moja au nyingine.
Meneja wa jukwaa hilo, Jackline Malavanu, anasema maelfu ya Watanzania wamepoteza fedha na kuathirika kisaikolojia kutokana na utapeli huo.
"Wengi huogopa kuzungumza kwa kuhofia kudharauliwa. Wengine hupitia msongo wa mawazo na kubaki kimya," anasema.
Kwa mujibu wa utafiti huo, visa vinane kati ya kumi vya utapeli hutokea kupitia mitandao ya kijamii, ambapo matangazo ya bei ya chini isiyo ya kawaida hutumika kuwavuta wateja. Baada ya kulipa fedha mapema, muuzaji hutoweka.
Malavanu anasema hali hiyo imechochea kuzinduliwa kwa kampeni ya 'Sema Upone', inayolenga kuwahamasisha waathirika kushiriki simulizi zao ili kuelimisha jamii na kuzuia wengine kuangukia katika mitego hiyo.
Jackline mwenyewe anasimulia kupoteza Sh. 660,000 alipokuwa mwanafunzi chuoni baada ya kuahidiwa simu ya mkononi kwa bei nafuu.
Baada ya kutuma fedha, aliombwa malipo ya ziada kwa madai ya ushuru, kisha mawasiliano yakakatika.
Mussa, mfanyabiashara wa mitindo, alipoteza Sh. 250,000 baada ya kuamini tangazo la bidhaa za mavazi.
Neema Mbaga, mwanafunzi wa sekondari, alipoteza Sh. 120,000 akitarajia kununua kompyuta ndogo ya masomo.
Hassan, mfanyabiashara wa kilimo, alipoteza Sh. 400,000 kupitia mteja bandia aliyedai amelipa kabla ya kupokea bidhaa.
Kwa wengi wao, hasara si fedha pekee. Ni kupoteza imani katika biashara ya kidijitali.
UCHUMI KIDIJITALI
Tanzania inaendelea kukuza uchumi wa kidijitali kwa kasi. Mitandao ya kijamii na majukwaa ya mtandaoni yamekuwa soko muhimu kwa vijana na wafanyabiashara wadogo.
Lakini iwapo udhibiti hautaimarishwa, utapeli na ukandamizaji vinaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika mifumo hii.
Wataalamu wa masuala ya fedha wanashauri wananchi kuwa makini na matangazo yanayoahidi riba ndogo kupita kiasi au bei zisizo halisi.
Wanasema ni muhimu kusoma masharti kwa kina, kuthibitisha usajili wa taasisi husika na kuepuka kutoa rukhsa ya kufikia taarifa binafsi zisizo za lazima.
Vilevile, mamlaka husika zinapaswa kuongeza ufuatiliaji na kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi na watu wanaokiuka sheria.
KUVUNJA UOGA
Kampeni ya Sema Upone inalenga kubadili utamaduni wa kunyamaza. Waandaaji wanahimiza waathirika kushiriki uzoefu wao kwa maandishi, sauti au video ili kuelimisha wengine.
Katika dunia ya kidijitali, taarifa ni kinga. Kadri simulizi zinavyowekwa wazi, ndivyo mitego inavyofichuliwa mapema.
Mikopo ya mtandaoni na biashara za kidijitali si adui wa maendeleo. Ni nyenzo muhimu za uchumi wa kisasa. Lakini zinahitaji uwazi, maadili na ulinzi wa watumiaji.
Bila hayo, ahadi tamu za dakika tano zinaweza kugeuka machungu ya miezi mingi - fedheha, deni na majeraha ya kisaikolojia.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED