Mgomi ahimiza Watanzania kuenzi tunu za waasisi wa Taifa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:40 PM Dec 10 2024

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farid Mgomi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farid Mgomi.

MKUU wa Wilaya ya Ileje, Farid Mgomi, amewaasa Watanzania kuendelea kudumisha na kuimarisha amani, upendo, umoja na mshikamano ikiwa ni tunu ya msingi wa maendeleo katika Taifa lililoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Hayati Sheikh Abeid Aman Karume.

Akizungumza mapema jana katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, lililofanyika katika Ukumbi wa Coommunity Center wilayani humo,  Mgomi amehimiza wananchi kuendelea kuzienzi tunu zilioachwa na waasisi wa Taifa hili. 

Amesema lengo ni kuhakikisha Tanzania inazidi kusonga mbele katika nyanja zote za maendeleo na kuwa mfano bora kwa Mataifa mengine.

Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya hiyo, ametoa pongezi kwa watumishi katika wilaya kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidi na kuhakikisha Wilaya ya Ileje, inasonga mbele kimaendeleo. 

Aidha amewasisitiza watumishi kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa kwa kila Mtu, hii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa wananchi pasipo kujali itikadi ya wananchi, dini, kabila au rangi. 

Aidha, Mgomi amewasisitiza wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili mmani, umoja na mshikamano viendelee kudumu nchini.