KIONGOZI wa chama cha upinzani cha National Democratic Congress (NDC), John Mahama ambaye alikuwa rais wa nchi hiyo kutoka 2012 hadi mapema 2017, ameibuka mshindi katika nafasi ya urais kwenye uchaguzi uliofanyika jana.
Kiongozi huyo amemshinda Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Mahamudu Bawumia aliyekuwa akiwania nafasi hiyo kupitia chama tawala cha New Patriotic Party (NPP).
Ushindi huo umetokana na zaidi ya wananchi milioni 18 wa Ghana walioshiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu nchini humo na kumchagua mrithi wa Rais Nana Akufo-Addo, ambaye anaachia ngazi baada ya kuitumikia mihula miwili.
Katika uchaguzi huo ambao ulifanyika juzi, wananchi pia waliwachagua wawakilishi wapya katika bunge la nchi hiyo.
Katika uchaguzi huo wagombea 11 wa vyama tofauti walijitokeza, na matokeo yalianza kutangazwa baada ya uchaguzi kumalizika na kura kuhesabiwa.
Ghana ina historia ya utulivu wa kisiasa, vyama viwili vikuu vya NPP na NDC vimepishana madarakani kwa amani tangu nchi hiyo iliporejesha demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992.
Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema serikali ya Ghana ilifunga kwa muda mipaka yote ya ardhini tangu Ijumaa usiku hadi jana ili kuhakikisha mchakato wa kura unaendelea vizuri.
AFP/AP/DW
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED