Mapya yaibuliwa polisi utata kifo cha daktari

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 11:30 AM Sep 16 2024
Mapya yaibuliwa polisi utata kifo cha daktari
Picha:Mtandao
Mapya yaibuliwa polisi utata kifo cha daktari

JESHI la Polisi limesema aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ulyankulu, wilayani Kaliua, mkoani Tabora, Dk. Dismas Chami (32), aliwahi kujaribu kujiua mara mbili kabla ya kifo chake chenye utata kilichoripotiwa mwishoni mwa wiki.

Vilevile, jeshi hilo limesema mwili wa daktari huyo anayedaiwa kupotea kisha kukutwa kichakani amefariki dunia katika eneo la Kombo Masai, Kata ya Malolo, mkoani humo, mwili ulikutwa umedungwa dripu yenye dawa ambayo bado haijafahamika.

Katika taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa juzi na Msemaji wa Polisi Makao Makuu Dodoma, DCP David Misime, ilieleza kuwa wanaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na wataalamu wengine ili kubaini chanzo cha kifo cha tabibu huyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wa awali juu ya kifo cha daktari huyo, alishajaribu kujiua mara mbili.

Jeshi hilo limesema kuwa Dk. Chami aliaga kwa mkuu wake wa kazi pamoja na mke wake Septemba 2, mwaka huu kuwa anakwenda mjini Tabora kushughulikia akaunti yake ya benki ambayo ilikuwa na changamoto.

Baada ya kuaga, jeshi hilo limeeleza kuwa Dk. Chami aliahidi kurejea siku iliyokuwa inafuata na ilipofika Septemba 4 mwaka huu, simu yake haikupatikana.  

"Septemba 10, daktari mkuu wa kituo hicho cha afya aliambatana na mke wa marehemu hadi kituo cha polisi kutoa taarifa ya kutokuonekana kwake," ilieleza taarifa hiyo.

Jeshi hilo lilisema kuwa siku hiyo hiyo walitoa taarifa kituo cha polisi, Dk. Dismas alimtumia mke wake ujumbe kupitia WhatsApp ulisema:

"Nisamehe sana, baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani, simamia kila kitu nilichoanzisha. Pesa zote zipo akaunti ya CRDB, simamia na watoto waseme, kwa heri."

Kamanda Misime alisema daktari huyo hakupatikana tena katika mawasiliano yake mpaka Septemba 13 majira ya saa tatu usiku, mwili ulipokutwa kichakani.