Kukamilika kwa nyumba za watumishi wa afya kuboresha huduma Peramiho

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:27 PM Dec 19 2024
Nyumba ya wafanyakazi wa Zahanati ya Mdundwaro katika kijiji cha Mdundwaro kata ya Peramiho wilaya ya Songea mkoani Ruvuma iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ikiwa imekamilika.
Picha: Faustine Feliciane
Nyumba ya wafanyakazi wa Zahanati ya Mdundwaro katika kijiji cha Mdundwaro kata ya Peramiho wilaya ya Songea mkoani Ruvuma iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ikiwa imekamilika.

Kukamilika kwa nyumba za watumishi wa afya katika Kijiji cha Mdundwaro, Kata ya Peramiho, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kumepunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za afya na vifo vya wananchi waliokuwa wakipoteza maisha njiani wakifuata huduma mbali na kijiji.

Wakazi wa kijiji hicho wamesema kuwa uwepo wa watoa huduma wa afya katika zahanati hiyo kwa muda wote umeimarisha upatikanaji wa huduma za afya.

"Awali, huduma katika zahanati hii zilitolewa kwa masaa, na mara nyingine watoa huduma walikuwa hawapo hasa mwishoni mwa wiki. Ilitubidi kusafiri kwenda Peramiho mjini au Songea, na wagonjwa wengi walipoteza maisha njiani. Sasa watoa huduma wapo hapa muda wote, hatuna haja ya kusafiri mbali. Tunashukuru kwa kukamilika kwa ujenzi wa nyumba za wauguzi na waganga," alisema Agustino Luhwoga, mkazi wa Kijiji cha Mdundwaro na Msimamizi wa Zahanati hiyo.

Mtendaji wa Kijiji hicho, Zawadi Mlapone, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba hizo, kisima cha maji, na matundu nane ya vyoo umeendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao umechangia kuboresha huduma za afya kwenye zahanati hiyo.

Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea, Hosana Ngunge (kushoto) akimuonyesha muuguzi wa Zahanati ya Mdundwaro, Sinasudi William alama ya uzinduzi wa ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa Zahanati hiyo. PICHA: FAUSTINE FELICIANE
"Kwa sasa tunaomba Serikali au TASAF watusaidie gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwasafirisha wagonjwa wanaohitaji matibabu zaidi katika hospitali kubwa za Peramiho au Songea. Hata hivyo, tunashukuru kwa hatua tuliyofikia," amesema Zawadi.

Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea, Ahosana Ngunge, amesema mradi huo ulianza mwaka jana baada ya maombi ya wananchi na umekamilika Machi mwaka huu.

"Mradi huu umegharimu shilingi milioni 179 ambazo zimetumika kujenga nyumba mbili za wafanyakazi wa kituo, matundu nane ya vyoo, kuchimba kisima, pamoja na ujenzi wa kichomea taka," amesema Ngunge.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Hassan Mtamba, ameishukuru TASAF kwa mradi huo na kuahidi kushirikiana na wananchi kutunza miundombinu yote pamoja na kutatua kero zilizobaki kwenye kituo hicho.