Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu ya Msingi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Wilson Mahela, amesema bila kuwa na walimu bora, majengo mazuri, vitabu, na vifaa vya kufundishia, mafanikio katika elimu hayawezi kupatikana.
Dk. Mahela alitoa kauli hiyo juzi wakati akifungua mafunzo ya matumizi bora ya vifaa vya TEHAMA kwa Waratibu wa Elimu na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Songwe, Iringa, na Ruvuma.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa walimu wakuu wanapaswa kuelewa changamoto zinazowakabili walimu wenzao na kuzitatua. Kwa kufanya hivyo, watajenga walimu bora watakaoongeza ufaulu katika shule zao.
"Tusipokuwa na uongozi mzuri, walimu wengine hawawezi kufundisha vizuri. Hali hiyo inaweza kutufanya tukose mafanikio tunayoyatarajia," alisema Dk. Mahela.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Dk. Mahela alisisitiza umuhimu wa TEHAMA katika elimu kwa kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia. Alisema kuwa walimu wanapaswa kuzingatia na kutumia mafunzo hayo ili kuimarisha uwezo wao wa kufundisha.
"Wanafunzi wa shule za msingi wanatakiwa kufundishwa TEHAMA ili wanapofika sekondari wawe na uelewa mzuri wa somo hilo, ambalo litawawezesha kujiajiri baadaye," alisema.
Aidha, aliongeza kuwa vijana wengi wamejiajiri kupitia TEHAMA, hivyo somo hilo linapewa kipaumbele ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na maarifa yanayowawezesha kushindana katika ulimwengu wa sasa.
Dk. Mahela alitoa wito kwa walimu kuhakikisha kuwa vifaa vya TEHAMA vinavyonunuliwa vinatumika ipasavyo na kuwanufaisha wanafunzi. Alisema kwamba hali iliyokuwepo awali, ambapo baadhi ya vifaa vilikuwa havitumiki, inapaswa kubadilishwa.
Mratibu wa Mradi wa Boost kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Laurence Raphael, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuboresha umahiri wa walimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa somo la TEHAMA.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kudhibiti Ubora wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Ephraim Simbeye, alisema kuwa baada ya mafunzo hayo, wizara itafuatilia maendeleo ya walimu walionufaika ili kuona matokeo yake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED