Kinana aonya viongozi kutoa ahadi ‘hewa’

By Halfani Chusi ,, Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 09:20 AM Apr 18 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.
PICHA: MAULID MBAGA
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, ameshauri viongozi wa serikali kuacha kuahidi mambo ambayo hayajawekewa mipango, au wasiyojua kuwa utekelezaji wake utafanyika lini ili kuepusha malalamiko yanayotolewa na wananchi.

Aidha, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kujituma na kufanyakazi kwa bidii huku wakiacha kujihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa.

Balozi Nchimbi pia, amewatembelea waathirika 50 wa mmomonyoko wa ardhi katika Mlima Kawetere, Kata ya Itezi jijini Mbeya na kuwakabidhi Sh. milioni 10.

Akizungumza na wananchi wilayani Bunda, mkoani Mara, Kinana amepokea malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali kuwataka wahame katika maeneo yao kupisha ujenzi wa mradi wa maendeleo, ambao walidai kuwa hawajalipwa hadi sasa licha ya kufanyiwa tathmini muda mrefu.

Wananchi hao wameonesha kukerwa na kitendo cha maeneo yao kuchukuliwa na nyumba zao kubomolewa pamoja na kupewa masharti ya kutofanya shughuli zozote za kimaendeleo katika maeneo hayo ikiwamo Kijiji cha Nyantwate.

"Viongozi wa serikali kabla ya kuwahamisha wananchi ni vyema wakaeleza ni lini ahadi hiyo itatekelezwa, kama ni watu kuhama watahama lini, na fidia watapewa lini, hakuna sababu ya kutoa ahadi halafu inakaa miaka na miaka, kila kiongozi anakuja anaahidi anaondoka."

Mwananchi wa kijiji cha Nyantwali, Saasita Mchanga, mmoja wa wanaohitaji kulipwa fidia baada ya kupisha mradi wa maendeleo, alisema wanateswa na ahadi hiyo huku akidai wanashindwa kujenga matundu ya vyoo kwenye shule iliyoko eneo hilo wakisubiri hatima yao ili wahame.

"Shule yetu vyoo vilishadondoka ukifika pale watoto zaidi ya 400 wanatumia labda matundu mawili, wananchi wa Nyantwali tunaomba kama bado hatujaondolewa basi turuhusiwe tufanye maendeleo kuwanusuru watoto wetu kwasababu kuna magonjwa ya milipuko," amesema Mchanga.

Kutokana na hali hiyo, Kinana amewashauri watendaji wa serikali kabla ya maamuzi yanayohusu kuhamisha watu, kufidia au kufanya jambo lolote linaloigusa jamii, wafanye utafiti wa kutosha wawe na uhakika, fedha zipatikane ndio watoe kauli, badala ya kutanguliza kauli kabla ya kutangaza fidia.

Amebainisha kuwa kumekuwa na tabia kwa viongozi kuwaambia wananchi wahame au wasilime katika maeneo yao halafu hakuna kinachoendelea.

Aidha, amesema anakumbuka wananchi hao waliahidiwa na mwaka jana mawaziri sita walikwenda katika eneo hilo wakiwa na usafiri wa helikopta na kuwataka watu wahame.

“Sasa walitoa ahadi bila kujiandaa na wamedanganya watu, leo wananchi wanakuja kuniuliza mimi sasa nitawajibu nini? Nataka kuwasihi hapa watendaji wa serikali kabla kuahidi kitu ni muhimu mkaanza kwanza kujipanga kuepusha usumbufu.

“Kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan wakati anawaapisha wakuu wa mikoa juzi, waende wahakikishe watu wanapewa haki yao, nitaongea na Waziri wa Fedha nimuulize vipi kuhusu malipo yenu aniambie kama imefika mwisho au bado,” amesema Kinana.

Katika hatua nyingine, Dk. Nchimbi amewataka wananchi kuendelea kuchapakazi kwa bidii, kufanyakazi zitakazowaingizia kipato kihalali na kujiepusha na rushwa kwa kuwa siku zote ndio adui wa haki. “Kuchapa kazi ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia kuwataka Watanzania wote kufanyakazi na ndipo tutazidi kulijenga taifa letu na kuimarika kiuchumi.”

Vile vile, amesema viongozi wa kitaifa wa CCM watendelea kuisimamia serikali kutimiza wajibu wake na kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025.