KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi amewasisitiza wananchi kulinda amani, kupinga udini, ukabila, ukanda pamoja na kutambue thamani ya taifa lao.
Kauli hiyo imeita leo wakati akizungumza na wananchi wa Kigoma Mjini, huku akisema hakuna shida kubwa kama kutangatanga kwenye nchi za watu kutafuta hifadhi.
Amesema amani ni jambo la msingi, na bila amani hakuna shughuli ambazo zitaweza kufanyika, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kutambua umuhimu na thamani ya utulivu wa kitaifa.
"Mfano Kigoma ni mkoa ambao unakambi nyingi za wakimbizi mnapaswa kuzingatia na kutambua kuwa wakimbizi hao wamekimbia nchi zao na kuja nchini Tanzania kutafuta hifadhi.
“Na watu hao wamekimbia nchi zao kwa ajili ya vurugu na ukosefu wa amani na hivyo amani inapaswa kulindwa sana nchini ili kila mmoja aweze kuishi kwa utulivu," amesema.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kulinda nyumbani kwao na kwamba wasiruhusu watu wakajaribu kuharibu amani iliyopo, akidai kuwa kuna watu wanalipwa kwa kuharibu amani iliyoko.
Amesema hakuna faida yoyote kama vurugu zitaibuka kwa sababu hawatafanya shuguli zozote kwa utulivu ikiwemo kilimo na biashara.
"Mkiwa mashambani mtalima kwa amani, mkiwa kwenye mifugo mtauza bidhaa zenu kwa utulivu, na mkiabudu misikitini na makanisani kwa utulivu endapo mkiwa na amani tu bila amani hamtafanya hivyo vyote.
“Miaka kadhaa iliyopita, hata umeme haukuwepo hapa, lakini sasa umeme umewaka, shule na zahanati zinajengwa, na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi unaendelea, nawaomba mzidi kushirikiana na viongozi walioko madarakani ili maendeleo yaendelee amani na utulivu ni msingi wa maendeleo,” amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED