Kigezo umri ajira chazua mjadala bungeni

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:35 AM Sep 03 2024
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ngwasi Kamani
Picha: Mtandao
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ngwasi Kamani

KIGEZO cha umri usiozidi miaka 25 katika ajira za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), zilizotangazwa hivi karibuni kimeibuliwa bungeni huku wabunge wakiishauri serikali kuondoa na kuangalia namna ya kuweka vigezo vitakavyoruhusu vijana wengi kuchangamkia fursa hiyo.

Agosti 31, 2024 taasisi hiyo ilitoa tangazo la nafasi za kazi 351 kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Suala hilo liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ngwasi Kamani ambaye aliomba Bunge kujadili hoja ya dharura na kubainisha kuwa kati ya vigezo vya waombaji kwenye nafasi hizo ni umri usiozidi miaka 25.

“Kwa elimu yetu ya kawaida mwanafunzi anamaliza elimu ya kidato cha nne akiwa na miaka 18 na akimaliza kidato cha sita 21 na akiingia chuoni anakwenda hadi miaka 24, lakini nafasi hizi umri usiozidi miaka 25, nafasi hizi ni chache na waombaji ni wengi ikiwezekana umri uongezwe ili vijana waliopo mtaani wanufaike,” alisema.

Alisema ni vyema umri uongezwe hadi miaka 30, ili kutoa fursa kwa vijana wengi kuomba na wasihukumiwe kwa umri.

Akifafanua hoja yake, Mbunge Kamani alisema kila mwaka wanaohitimu vyuo ni kuanzia 100,000 hadi 300,000 na nafasi za kazi ni chache.

Kutokana na hoja hiyo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alimpa nafasi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala, George Simbachawene, ambaye alisema katika umri huo ni kigezo cha majeshi ili wanaochukuliwa wawe na ukakamavu.

“Tunafahamu kwamba nafasi zilizotangazwa sio za wahitimu tu, hawa tunahitaji ambao wataenda kupewa mafunzo porini na ndio maana wanachukua watu wenye umri usiozidi miaka 25, kwa sheria yetu ya utumishi wa umma ni umri usiozidi miaka 45 hivyo tukichukua wa miaka 45 hakika hataweza mafunzo haya ya kijeshi,” alisema.

Waziri Simbachawene alisema tangazo linawahitaji wa kada za kawaida na kwamba lazima wapite mafunzo ya kijeshi na umri huo ni kigezo cha kupima ukakamavu.

Aliahidi serikali itachukua maoni ya wabunge na kuyafanyia kazi.

Hata hivyo, kutokana na majibu hayo Spika Tulia alitoa fursa kwa wabunge kujadili ili kuishauri serikali.

“Jambo hili si mara ya kwanza kujitokeza bungeni kuhusu vigezo vya ajira, maeneo ya jeshi na jeshi usu na tulisema kwasababu ya jeshi wana vigezo vya ziada, lakini tulishashauri na kwa kuwa linakwenda na kurudi ni vyema serikali ipate ushauri,” alisema Spika.

WALICHOSEMA WABUNGE

Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Noah Saputu, alisema suala la umri hata kama ni jeshi usu ni vyema wataalamu wakatafakari hali za Watanzania na vijana waliopo mtaani kwa kukosa ajira.

“Hiki kigezo cha umri hakipo sawa kwasababu Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na jeshi usu mafunzo hayawezi kufanana, suala la umri liwe hadi miaka 30, suala la afya likajulikane kwenye mafunzo huko baada ya kupimwa, kuweka miaka 25 ni kuwazuia vijana wengi kupata ajira,” alisema.

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, alisema umri uongezwe watu waombe kama ni suala la mazoezi mtu ashindwe mwenyewe.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda, alisema kuweka umri wa miaka 25 kutawaweka vijana wengine nje, kwa kuwa ni muda mrefu ajira hazijatoka.

KAULI YA SPIKA

Baada ya maoni ya wabunge, Spika Tulia alisema; “Nakumbuka tulisema kwa upande wa jeshi kwasababu wana vigezo vya ziada waache hivyo na hizi taasisi nyingine ziangalie ambazo hazihitaji hiki kigezo cha watu kupitia mafunzo hayo.

Alisema kwa kuwa Mbunge mwenye hoja hajatoa azimio la kuazimiwa na Bunge, serikali ichukue ushauri wa wabunge kwa yale yanayoweza kurekebishika yarekebishwe.

“Kwa mfano haya ya dereva wa JWTZ hawezi kulingana na wa TAWA, ukitaka kuweka vigezo sawa ni bora tuwapeleke wote sasa wakapate mafunzo ya jeshi halafu watawanywe kwenye majeshi,” alisema.

Alisema serikali ione utofauti ili isiwaondoe kwenye mfumo wa ajira na kwamba kuna mambo yanazungumzika na waweke mazingira kuwa kwa aina ya mafunzo ambayo mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 25 anaweza, apewe fursa.