Keissy aonesha nia ya kurudi bungeni

By Mussa Mwangoka , Nipashe
Published at 12:04 PM Oct 03 2024
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy.
Picha: Mtandao
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy.

MWANASIASA machachari na aliyewahi kuwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy, ameonyesha nia yake ya kugombea tena ubunge katika jimbo hilo baada ya kuangushwa mwaka 2020.

Keissy amesema dhamira yake ya kugombea ubunge kwenye jimbo hilo iko pale pale licha ya jimbo hilo kuongozwa na mbunge kutoka upinzani.
 
Katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipoteza kiti cha ubunge katika jimbo hilo baada ya mbunge wa sasa, Aida Khenan, kumbwaga Keissy aliyekuwa katika kwenye nafasi hiyo kwa vipindi vitatu mfululizo.

 Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka Sumbawanga mkoani Rukwa, Keissy alisema nia yake ya kugombea ubunge kwenye jimbo hilo haijabadilika kwa kuwa  haoni kitu kipya kinachofanywa na mbunge wa sasa.

 "Nataka kurudi kugombea kwa kuwa mbunge aliyepo hivi sasa hakuna cha tofauti alichofanya. Nilikuwa  nimebuni miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi wa Nkasi Kaskazini lakini michache tu ndiyo ametekeleza na mingine bado. Kero  bado ni nyingi, hivyo kuna umuhimu wa kurudi tena," alisema. 

Hata hivyo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi ni miradi ipi ambayo mbunge wa sasa  ametekeleza, hakuwa tayari kufanya hivyo, badala yake alieleza nia yake ni kugombea tena ubunge ili kutatua kero za wananchi ambazo ni ukosefu wa maji safi na salama na barabara za vijijini.

 Hadi sasa, Jimbo la Nkasi Kaskazini linaonekana kuwa lulu kwa wana CCM wengi wanaonyemelea kugombea ili kumng’oa Kenani. Hadi sasa kuna watu takriban 20 wanatajwa kuwania jimbo hilo akiwamo Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukara. 

Khenani alishinda ubunge baada ya kupata kura 21,226 na kumshinda Keissy wa CCM ambaye alipata kura 19,972. 

Keissy anakumbukwa kwa matukio kadhaa akiwa bungeni likiwamo la kunusurika mara mbili kupigwa na wabunge wa Zanzibar, huku wakimtolea lugha za kejeli na matusi.

 Keissy aliwahi kujenga hoja akieleza udhaifu wa katiba ya nchi katika suala la Muungano baada ya kutoa maneno yaliyodaiwa kuwa ya kashfa kwa wabunge wa Zanzibar wakati wa akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

 Tukio lingine ni wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba. Alinusurika pia kupigwa baada ya kupinga Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano.
 
 Akichangia mjadala wa Katiba, mbunge huyo asiyeisha vituko, alisema  haiwezekani Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kwa kuwa hakuchaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara jambo lililozua tafrani bungeni.