KANISA la Kiaskofu la Anglikana duniani (ACC), lenye makao yake makuu nchini Marekani, limeahidi kushirikiana na serikali katika kuboresha sekta ya Afya, Elimu na Maji kwa kujenga miundombinu itayowasaidia wananchi kupata huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Padri wa Kanisa hilo Canon Freeman akimwakilisha Askofu Mkuu wa Kanisa hilo duniani, Mark Haverland, amesema wameamua kuanzisha kanisa hilo ili kurudisha misingi thabiti ya imani ambayo iliasisiwa kabla ya ukoloni.
Amesema licha ya kuanzisha kanisa hilo kwa lengo la kukufua na kuendeleza misingi ya imani kuhusu kanisa hilo, pia watakuwa bega kwa bega kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumzia kuhusu masharti ya kanisa hilo kutoa misaada kwenye jamii, Freeman amedai hawana vizuizui kusaidia wananchi kwani wao ni miongoni mwa wanaopinga vitendo vya unyonyaji na ushoga.
“Tumeamua kuanzisha kanisa hili duniani ili kurejesha misingi ya kanisa la Anglikana, iliyokuwepo awali kabla ya ukoloni, jukumu letu ni kutangaza neno la Mungu na kuwaletea maendeleo wananchi wetu,” amesema Padri Freeman.
Askofu wa Kanisa hilo nchini Tanzania, Elibariki Kutta, amesema septemba 15 mwaka huu atakabidhiwa rasmi majukumu ya kuongoza kanisa.
Amesema mambo manne watakayoyasimamia ni Ibada kuhakikisha wanawahubiria watu habari njema ya wokovu na kuishi katika misingi sahihi ya imani, aidha kutenda haki kuwapatia stahiki na mafao watumishi wote wataohudumu ndani ya kanisa hilo.
Ameongeza kuwapatia maendeleo wananchi, kuwajengea vituo vya afya, shule na miradi ya maji hususani wananchi waishio vijijini ambao ndio ukabiliwa na uhaba kubwa wa huduma hizo, hutumia umbali mrefu na gharama kubwa kuzifuata maeneo mengine pamoja Imani ambayo aliitafsiri kama kuishi misingi ya kanisa la Anglikana.
Amesisitiza kuwa kanisa hilo, limeweka utaratibu mzuri wa sadaka zinazotolewa kuwanufaisha waumini, alieleza kuwa kila eneo litakuwa na mamlaka ya kutumia sadaka zinazotolewa kuamua kufanya shughuli za maendeleo walizozipanga.
Amesema uhuru huo ni mzuri kwa sababu unawapa mamlaka waumini kupanga na kuweka vipaumbele vyao kulingana na sadaka inayopatikana katika eneo husika la kanisa.
“ Tumeona kuna unyonyaji mkubwa kwenye sadaka zinazotolewa makanisani, utaratibu wa sadaka kuchukuliwa na uongozi wa juu sio mzuri, sisi tumekuja na mtindo wa kwamba kila kanisa litakuwa na maamuzi katika kila fedha inayokusanywa,” amesema Kutta.
Mlezi wa wanawake wa kanisa hilo, Norah Kutta, amesema wanakwenda kufufua misingi ya kanisa na kuimarisha uchumi wa kila mwanamke ambaye ndio kiungo muhimu katika maendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED