MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, amesema kuwa pamoja na watu wengi kufunga kutokana na sababu mbalimbali katika jamii, kubwa ikiwa ni kutokana na imani hususan wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa na Kwaresma, lakini ni afua ya afya.
Profesa Janabi, mwanataaluma, tabibu na bingwa aliyebobea kwenye magonjwa yaliyomo kwenye kundi la NCDs, hajutii kuwa na mlo mmoja au miwili kwa siku, akizitaja kuwa kati ya tiba ya kuondoa mabaki yasiyohitajika mwilini.
Katika kitabu chake: Mtindo wa Maisha na Afya Yako, anatoa elimu kwa umma kuhusu mbinu za kufunga na faida zake (intermittent fasting), akisema wanaofunga wanaongeza siku za kuishi; wana uzito unaowiana; wanapunguza kalori na kuokoa muda.
Prof. Janabi anazitaja faida nane za kiafya kwa mtu anayefunga, akisema ni afua muhimu katika afya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Miongoni mwa sababu za kiafya ukifunga ni kati ya hizi; Kupunguza uzito. Kufunga ni afua inayopunguza uzito na inaweza kuwa njia nzuri ya kupambana na uzito uliopitiliza. ldadi kubwa ya watu hutumia njia hii kupunguza uzito.
Ingawa kwa kundi hili ni muhimu kujiuliza kwa nini wanaongezeka uzito, ili kuzuia visababishi vitakavyowafanya kuwa na uendelevu wa kudumu, ni muhimu kujua kiini cha uzito ni nini. Watu wengi wanashindwa kutambua hasa nini chanzo cha kuongezeka uzito.”
Anasema pamoja na kufunga kuwa sababu ya kupungua uzito, ni vyema anayehitaji kupungua uzito kuzingatia sababu za kuongezeka kwa uzito.
Anaitaja faida ya pili ya kufunga kuwa ni; Ukinzani wa wingi wa insulini mwilini (Insulin Resistance).
“Ili kuweza kutumika kwa ajili ya kuupa mwili nguvu, chakula humeng'enywa na ili kufanywa kuwa katika chembechembe rahisi kuchakatwa ili kuzalisha nguvu na viini lishe kuujenga mwili.
Vyakula vyenye asili ya wanga (carbon hydrates) au sukari na kwa uchache sana protini, kikishaingia mwilini, kiungo cha mwili kinachoitwa kongosho (pancreas) hutoa kichocheo cha insulini.
Kongosho, ni kiungo maalumu ambacho kazi yake ni kuzalisha insulini. Insulini inafanya kazi ya kuchukua sukari au wanga uliozidi na kuhifadhi kama mafuta. Kwa kawaida sukari na wanga huhifadhiwa katika sehemu mbalimbali mwilini kama vile kwenye ini, misuli au tumbo (kitambi).
Ikiwa mwili utapokea kiasi kikubwa cha wanga na mafuta zaidi ya kinachohitajika, kinaongeza mzigo mkubwa kwa kongosho katika uzalishajl wa insulini.”
Anasema mzigo mkubwa kwa kongosho matokeo yake ni kusababisha kushindwa kwa insulini kuhimili kazi yake na sukari au mafuta vinabaki katika mifumo yake katika mishipa ya damu na hali hiyo ya uzalishaji wa insulini nyingi isiyofanya kazi kama inavyotakiwa, husababisha kutokea kwa ukinzani wa insulin.
Hali hii inaweza kuwa ndio hatua ya kuingia kwenye matatizo ya kisukari aina ya pili ambayo hutokana na mabadiliko ya mwili, mfumo na ulaji. Tofauti na aina ya kisukari cha kuzaliwa nacho.”
“Takwimu za kitabibu zinaonyesha kuwa watu tisa kati ya 10, wana ukinzani wa insulini bila ya kujitambua. Kitaalamu, mwili unapokuwa na ukinzani wa insulini uzito wa mwili unaongezeka.
Jambo hili ni muhimu kwa kuwa ndio moja ya sababu kubwa ya kuongezeka uzito wa mwili. Watu wenye kisukari aina ya pili (Type lI Diabetes) wanaotumia vidonge uzito wao upo juu kwa sababu insulini ipo juu mwilini mwao.
Moja ya kazi kubwa ya insulini mwilini ni kutunza chakula (kuweka akiba) katika mfumo wa mafuta. Kwa maana hiyo, insulini inageuza sukari na wanga kuwa mafuta na kuhifadhi mwilini hali inayosababisha ongezeko la uzito.
Kwa maana hiyo basi, tunaweza kusema uzito ni matokeo ya ukinzani wa insulini.”
Bingwa huyo wa Magonjwa ya Moyo mwenye shahada tatu katika sayansi ya tiba, anasema kufunga ni mbinu ya kukiepuka kisukari.
Sukari ikiwa sawa inaweza kusababisha mabadiliko ya matibabu wanayopata, kupungua kwa vidonge, sindano na dozi wanazopata au hata kusimamishwa kutumia dawa kabisa na kutumia chakula kama tiba.
Kisukari (Diabetes Mellitus Type 2) ni ugonjwa wa lishe na tiba yake kuu lazima iwe lishe. Hali hii huwapa unafuu kutokana na madhila ya kisukari. Afua hii ikitumika vyema na kwa uangalifu, inaweza kupunguza tatizo kubwa la sukari.
Kwa wale waliopo katika hatua za awali za kisukari (pre-diabetes), afua hii inaweza kuongeza muda mrefu kabla ya mtu kuwa mgonjwa kamili. Lakini inaweza kuipa kongosho afueni na hivyo kurejesha afya na kuwa nzima.
Upo ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuponywa kwa watu wanaoishi na kisukari, au waliopo katika hatua za awali kupona kwa kuzingatia afua hii kwa uangalifu na ufuatiliaji wa karibu wa afua hii na afua nyingine.”
TAKWIMU ZA NCDs
Takribani vifo nusu milioni ambavyo vingeepukika, hutokea kila mwaka. Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema.
Nchini Magonjwa Yasiyoambukizwa (NCDs), huchangia takribani asilimia 70 ya magonjwa mengine kama vile figo na moyo. Asilimia tisa ya Watanzania wanaugua kisukari huku asilimia 15 wakiugua presha, kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED