India yaonyesha nia duru ya tano ya kunadi vitalu

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:46 PM May 15 2024
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mha. Danstan Asanga (wanne kushoto) akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya PURA na Ujumbe wa Ubalozi wa India Nchini Tanzania.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mha. Danstan Asanga (wanne kushoto) akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya PURA na Ujumbe wa Ubalozi wa India Nchini Tanzania.

UBALOZI wa India nchini Tanzania umekutana na kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kupata taarifa zaidi kuhusu kazi ya kunadi vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia linalotarajiwa kufanyika Tanzania Bara mwaka huu.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, katika Ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu wa Pili wa Balozi wa India Nchini Tanzania anayeshughulikia masuala ya Biashara, Narender Kumar na Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa PURA, Danstan Asanga.

 Akizungumza katika kikao hicho, Kumar alisema kuwa baada ya kusikia mpango wa serikali wa kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia kupitia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2024/25, Ubalozi wa India Nchini Tanzania uliona vema kukutana na Mamlaka hiyo ili kufahamu kwa mapana kuhusu suala hilo ili kupata taarifa kamili kwa kampuni na wadau nchini India. 

"Ni matumaini yetu kuwa kampuni kutoka nchini India zitavutiwa na taarifa hii ndio sababu tumeamua kutafuta taarifa zaidi zitakazowasaidia katika kufanya uamuzi wa kushiriki katika kazi ya kunadi vitalu na hatimaye kuwekeza katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini Tanzania" alisema Kumar.

Akitoa maelezo kuhusu duru ya tano ya kunadi vitalu, Asanga alisema kuwa PURA, kwa niaba ya serikali, imeendelea na maandalizi ya kazi hiyo na kwamba tayari shughuli mbalimbali zimekamilika ikiwamo maandalizi ya mkataba Kifani wa uzalishaji na ugawanaji wa mapato ambao umewasilishwa Wizara ya Nishati kwa hatua zaidi.

Kazi nyingine zinazofanyika ni pamoja na uwekaji wa mipaka ya vitalu vitakavyoingizwa katika mnada mara baada ya kupata ridhaa ya Wizara ya Nishati na maandalizi ya vifurushi vya data za petroli.

Asanga alisema kuwa mapitio ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 yanaendelea ili kuangalia vifungu vya sheria vinavyohitaji maboresho na kwamba PURA inashiriki kwenye mapitio hayo. 

Asanga alisema kazi ya kunadi vitalu itafanyika baada ya kukamilika kwa maandalizi ya msingi ikiwamo mapitio ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 na kwamba mpango wa serikali ni kuzindua duru hiyo mwaka huu. 

Mbali na kujadili duru ya tano ya kunadi vitalu, PURA na Ubalozi wa India Nchini Tanzania, zimejadili pia uwezekano wa kuanzisha mashirikiano baina ya mamlaka za udhibiti wa utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania na India.

Jambo jingine lililojadiliwa na pande hizo ni uwezekano wa kushirikiana katika programu za kujenga uwezo kwa watumishi katika masuala ya mafuta na gesi asilia kupitia ufadhili wa serikali ya India.