Hoja nne zilizotikisa Muungano 2023/24

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:46 PM Apr 25 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo, amesema katika kuimarisha na kulinda Muungano kwa kipindi cha mwaka 2023/24 pande zote mbili zimekuwa kwenye majadiliano ya kumaliza hoja nne ambazo hazijapatiwa ufumbuzi.

Dk. Jafo amebainisha hayo bungeni wakati akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2023/24 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25.

Ametaja hoja hizo kuwa ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Zingine ni mapendekezo ya tume ya pamoja ya fedha, usajili wa vyombo vya moto na uingizaji wa sukari kutoka Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.

Amesema katika kujadili hoja hizo kwa kipindi cha mwaka 2023/24, ofisi hiyo  imeratibu vikao vitatu vya kamati ya pamoja ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzani (SJMT) na SMZ ambako vikao hivyo ni pamoja na cha makatibu wakuu wa SJMT na SMZ kilichofanyika Dar es Salaam Septemba 22, 2023.

Kingine ni kikao cha mawaziri wa SJMT na SMZ kilichofanyika Zanzibar Machi 5, 2024; na kikao cha kamati ya pamoja ya SJMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano ambacho mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais wa JMT kilichofanyika Zanzibar Machi 6, 2024.

“Wizara zenye hoja zimepewa maagizo ya kuzipatia ufumbuzi na napenda kulihakikishia bunge kuwa serikali zote mbili zina nia ya dhati na thabiti katika kuhakikisha hoja za Muungano zilizopo na zitakazojitokeza zinashughulikiwa kwa ushirikiano mkubwa ili kuulinda na kuudumisha Muungano wetu adhimu,” amesema.

Pia amesema ofisi imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu na faida za Muungano kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na kwenye maonyesho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) na maadhimisho ya Wiki ya Vijana.

Kadhalika, amesema wanaendelea kuratibu masuala 22 ya Muungano yanayosimamiwa na wizara, taasisi na idara za Muungano kwa faida ya pande zote mbili.

“Hadi kufikia Machi, 2024 taasisi 33 kati ya 39 za Muungano tayari zina ofisi Zanzibar, hivyo kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Ofisi imeendelea kuhimiza taasisi zilizosalia kukamilisha ufunguzi wa Ofisi zao Zanzibar,” alisema Dk. Jafo

MASUALA YA UCHUMI

Dk. Jafo amesema ofisi hiyo imeendelea kuratibu gawio kwa SMZ kwa kila mwaka na hadi kufikia Machi, 2024 zaidi ya Sh. bilion 91.465 zilipelekwa Zanzibar zikijumuisha misaada na mikopo nafuu ya kibajeti kutoka nje Sh. bilion 72.965.

Amesema gawio lingine ni kutokana na faida ya BoT Sh. bilioni 4.5 na fedha zitokanazo na makato ya mishahara ya watumishi (PAYE) wa Zanzibar wanaofanya kazi Tanzania Bara Sh. bilioni  14.

Jafo ameomba bunge kupitisha bajeti ya Sh. bilioni 31.8 kwa mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 10.43 ya bajeti ya mwaka 2023/24 ambayo ilikuwa Sh.bilioni 28.8.