Hoja nne za Mchome alizofikisha kwa Msajili kuhusu CHADEMA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:20 AM Mar 27 2025
news
Mtandao
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembruce Mchome

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembruce Mchome amesema maamuzi ya kukilalamikia chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ulitokana na kutokuridhishwa na majibu ya Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Mchome ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA amebainisha hayo leo Machi 26 wakati akizungumza na Nipashe Digital juu ya uamuzi huo huku akitaja hoja nne alizoziwasilisha mbele ya msajili baada ya kutokuridhishwa na majibu ya chama chake.

Amesema barua hiyo aliyoiandika Machi 15, 2025 pamoja na mambo mengine ilikuwa na ombi la kumtaka achunguze kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kilichofanyika Januari 22, 2025.

“Achunguze kupitia kumbukumbu za kikao hicho kuanzia orodha ya wajimbe waliokuwepo, ajenda za kikao na mwenendo mzima wa kikao,” amesema.

Aidha, amesema baada ya hapo alimuomba Msajili kutengua uteuzi wa wajumbe wote wa kamati kuu uliofanyika kwenye hicho kikao pamoja na kutengua maamuzi yote yaliyowahi kufanywa na kamati kuu kuanzia Januari 22 hadi leo.

“Baada ya hapo nimemuomba amuelekeze Katibu Mkuu John Mnyika kuitisha baraza kuu la chama ili tuweze kurudia zoezi hilo la uthibitishwaji,” amesema Mchome.

Hata hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia barua ya Naibu Msajili, Sisty Nyahoza imetoa wiki moja kwa CHADEMA kujibu malalamiko ya mjumbe huyo wa Baraza Kuu, Mchome. 

Nyahoza, imeitaka amekitaka Chama hicho cha CHADEMA kujibu malalamiko hayo kabla ya Machi 31, 202

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mnyika amezungumza na Nipashe Digital na kueleza kuwa uteuzi huo ulifuata kanuni na Katiba ya chama hicho na kwamba hakuna kilichovunjwa, huku wakiona kinachofanyika kinalengo la kuwatoa kwenye msitari wa ‘No Reforms No Election’ (hakuna uchaguzi bila mabadiliko).