Fursa kedekede ziara ya Samia Uturuki

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:46 AM Apr 18 2024
RAIS Samia Suluhu Hassan.
PICHA: IKULU
RAIS Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameanza ziara yake leo, nchini Uturuki kwa mwaliko wa kiongozi mwenzake, Rais Recep Tayyip Erdogan.

Miongoni mwa majadiliano yenye vipaumbele ni kuimarisha uhusiano, elimu na fursa kibiashara kati ya nchi hizo, ambayo imekua kutoka dola milioni tisa za Kimarekani miaka sita iliyopita na kufikia milioni 22, mwaka jana.

Rais Samia, anatarajiwa kutia saini makubaliano kwenye maeneo sita kati ya 10 yaliyo katika mkakati, ikiwamo ufadhili wa masomo elimu ya juu, teknolojia, kuhifadhi nyaraka, sayansi pamoja na ubunifu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, kabla ya ziara hiyo, amesema imeanza leo hadi Aprili 21 ni ya kipekee ikizingatiwa haijafanyika kwa miaka 14.

Makamba, amesema wakati Rais Samia akiwa nchini Uturuki, atapata fursa ya kuhudhuria kongamano la biashara na uwekezaji litakalofanyika mjini Istanbul, kuongeza wigo wa uwekezaji nchini na soko katika nchi hiyo.

"Kuna maeneo ambayo tunawekeana hati za makubaliano, mpaka hususan sita, tutaingia mikataba hasa elimu ya juu, kuhifadhi nyaraka, sayansi, teknolojia. Urari wa biashara kati ya nchi zetu, Uturuki wanauza zaidi kwetu kati ya dola 250,000.

"Miaka sita iliyopita biashara imepanda, mwaka jana, biashara ilifikia dola milioni 22 ukilinganisha na dola milioni tisa miaka sita iliyopita," amesema Makamba.

Amefafanua ukubwa wa uchumi wa nchi hiyo, ambao ni miongoni mwa nchi za barani Ulaya, ikiwa kati ya zilizo tajiri duniani, hivyo ziara hiyo ni muhimu na yenye tija kwa taifa.

"Tuna fursa kubwa ya kiteknolojia, kutoka kwao. Biashara kubwa kutoka Tanzania kwenda Uturuki ni mazao na vito. Tutaangalia maeneo mapya ya ushirikiano na dhifa, iliyoandaliwa na mwenyeji wake," ameongeza Makamba.

Kadhalika, biashara kubwa kutoka Tanzania, kwenda nchini Uturuki ni kahawa, nazi, tumbaku ghafi, minofu ya samaki, mchele na maharagwe, ambayo huuza bidhaa hizo kwa wastani wa dola milioni 15,99 kwa mwaka.

Pia kwenye uwekezaji wa kampuni za Uturuki uapande wa Tanzania bara, ni takribani dola milioni 414.23 katika sekta ya usafirishaji, uzalishaji, na utalii na ajira zinafikia 6,062.

KUTUNUKIWA UDAKTARI

Baraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki, limeamua kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan shahada ya heshima ya udaktari katika uchumi.

Uamuzi huo wa baraza ni kutambua uongozi wake wa kipekee, ambao umeleta mageuzi kijamii, kisiasa na kiuchumi Tanzania. 

Mageuzi hayo yameboresha ustawi wa Watanzania, kuimarisha sifa ya Tanzania duniani, kukuza uhusiano kibiashara, kiuchumi, kisiasa kati ya Tanzania na nchi zingine, ikiwamo Uturuki.

Hafla ya kukabidhiwa tuzo hiyo inafanyika leo katika Chuo Kikuu cha Ankara, ikiongozwa na Prof. Necdet Ünüvar ambaye Mkuu wa Chuo hicho. Hafla hiyo itahiduriwa na wanataaluma na wanafunzi wa chuo hicho na mabalozi wa nchi za Afrika, wanaowakilisha nchi zao Uturuki.