Duni achambua matatu magumu hatosahau siasa, uchaguzi Z’bar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:01 AM Sep 05 2024
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji
Picha;Mpigapicha Wetu
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema amepitia mito, milima na mabonde ya kisiasa ambazo hatasahau maishani mwake, ikiwamo kushitakiwa kwa kosa la uhaini.

Duni aliyasema hayo jana katika hafla ya kutunukiwa zawadi na chama chake kutokana na utumishi wake na sasa amebaki kuwa mlezi na mshauri wa ACT Wazalendo.

Alisema baada ya kushtakiwa kwa uhaini na kuwekwa gerezani kwa miaka minne, alipoteza wazazi wake wawili akiwa huko bila kushuhudia maziko yao.

“Jambo kubwa ambalo limenipata ambalo nikilikumbuka huwa ninasikitika ni wakati wa kesi ya uhaini. Wakati tunapandishwa mahakamani pale Vuga, mzee wangu, yaani baba yangu mzazi, alikuja kuniona kwa lengo la kunisalimia.

“Lakini jambo la kusikitisha mzee wangu hakupewa ruhusa na alipigwa na mmoja wa askari na akaanguka, huku nikiwa ninashuhudia na wala sijamwona tena mpaka amefikwa na mauti. Sikuruhusiwa kwenda kumzika. Kwa  kweli mengi yananisikitisha, lakini hili ni gumu sana,” alisema.

Duni alitaja jambo lingine kuwa ni Wazanzibari imekuwa kama utamaduni kila miaka mitano kuuawa kwa sababu ya uchaguzi. Alisema kila anapopata nafasi ya kuonana na viongozi wa kitaifa bila hofu wala kuogopa, amekuwa wakiwaambia kuhusu suala hilo.

“Huwa nawaambia hivyo jamani hakuna njia nyingine yoyote isipokuwa kuuana? Wazanzibari haiwezekani kufanya uchaguzi ukawa salama? Hivi tumelaaniwa sisi Wazanzibari, maana duniani kote watu wanagombana  lakini hufikia siku watu hurudi katika meza wakazungumza na humaliza tofauti zao,” alisema.

Duni alisema anashangaa kuona kuna muafaka wa maridhiano inafanyika Zanzibar kwa ajili ya kumaliza tofauti zao, lakini kila inapofika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, huwa yanajitokeza mauaji makubwa, jambo hilo limekuwa likimkereketa, licha ya kusema kuwa anaamini kuna siku mambo hayo yataisha.

Alisema ili kuondokana na janga hilo ni lazima kushikamana na kuondokana na siasa za chuki na uhasama ambapo Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume, alihakikisha kujenga umoja wa Wazanzibari na alifikia hatua ya kutukanwa kwa kuanzisha ndoa za makabila ili kuwaunganisha.

Jambo lingine ambalo hatalisahau, alisema ni baada ya kufariki dunia kwa mwanasiasa mkongwe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na chama kupita  katika misukosuko mikubwa.

Misukosuko hiyo  aliitaja kuwa ni pamoja na kumpata mrithi wake katika nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais na mrithi wa mwenyekiti wa  chama na yote hayo walifanikisha.

Alitaja jambo lingine ni uchaguzi mkuu wa chama wa kupanga safu za uongozi. Katika mchakato huo, alisema alipigwa majungu,lakini alifanikisha kusimamia akiwa katika nafasi ya mwenyekiti na hatimaye safu kamili na imara ya uongozi ikapatikana.

Duni alikishukuru chama chake kwa kitendo walichokifanya jana cha kumpatia  zawadi na kuendelea kumuenzi akiwa bado yuko hai kwa sababu ni bahati kubwa kwake ya kukirimiwa.

Alisema baadhi ya viongozi wenzake waliokuwa pamoja katika mapambano, washatangulia mbele ya haki na hawakupata bahati hiyo, hivyo anajiona mwenye  bahati kubwa.

Aliwataja wenzake hao ni Shabani Mloo, Maalim Seif Sharif Hamad na Masoud Yussuf Mgeni  ambaye alikaa naye jela kwa muda wa miaka mitatu. Wanasiasa hao kwa sasa wote ni marehemu.

Pia alimshukuru mke wake kwa kumvumilia muda wote aliopata misukosuko ya kisiasa hasa pale alipokuwa gerezani kwa muda wa miaka minne na kumlelea familia yake ikiwamo wazazi wake Mzee Duni hadi kuwazika.

Hata hivyo, Duni alisema licha ya kushawishiwa kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini hana mpango huo.

“Sijafikiria wala sijadhani na wale wanaodhani kwamba Babu Duni anakwenda CCM. Mie?”alisisitiza.

Mwenyekiti wa chama hicho,  Othman Masoud Othman, alisema dhamira ya  kumuenzi Duni ni kuendelea kupata elimu ya uongozi kutoka kwake na kuwataka vijana kuwa mfano kwa mwanasiasa huyo ambaye alipagania haki na uadilifu ,hivyo vijana wasichoke kupigania haki yao mpaka itakapopatikana.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  alisema katika maisha ya Duni, amejifunza ujasiri wa kufanya jambo bila kutaka sifa.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alisema siku hiyo ni ya kipekee ya kutoa majibu kwa vitendo kuwa ACT Wazalendo ni chama kinachotekeleza siasa safi ndani na nje ya chama.

Makamu Mwenyekiti wa chama Zanzibar hicho, Ismail Jussa Ladhu, alisema Duni amepita katika nyayo za Maalim Seif za kujitambua kwa anachokisimamia na hajawahi kubadilisha msimamo wake kuhusu Zanzibar na uzanzibari jinsi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar usivyo wa haki kwa Zanzibar.

Alisema mtu anayejitambua huwa habadiliki ovyovyo na Juma Duni amepata heshima kubwa kwa wanachama wa ACT kutokana na kujiitambua kwa sababu hajawahi kubadilisha msimamo wake.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Isihaka Mchingita, alisema historia mara nyingi hukumbuka watu baada ya kifo chao, lakini chama kimeamua kuyaenzi maisha ya Duni akiwa hai.

Alisema amejifunza vitu vingi kutoka kwa mwanasiasa huyo ikiwamo ustahamilivu, kusimama katika njia imara na mwanasiasa mahiri ni yule anaepigania hatma ya taifa lake.

Katika hafla hiyo, Duni alikabidhiwa zawadi mbalimbali zikiwamo fedha, samani na gari aina ya Toyota Prado.