Changamoto wanafunzi kutembea umbali mrefu yapatiwa suluhu Hai

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 02:19 PM Feb 21 2026
news
Picha Mpigapicha Wetu
Changamoto wanafunzi kutembea km 18 yapatiwa suluhu Hai

CHANGAMOTO ya wanafunzi katika Kijiji Cha Mbatakero wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, kutembea umbali wa kilomita 18 kwenda shule, sasa imekwisha baada ya kuzinduliwa kwa shule mpya ya sekondari Mbatakero iliyopo kijijini hapo.

Mmoja wa wananchi Lucy Wilbert amesema hayo Februari 21 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba aliyefika kutembelea, kukagua na kuzindua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Mbatakere.

Lucy amesema pamoja na umbali wa kwenda shule pia baadhi ya wanafunzi walikatisha masomo kutokana na mimba za utotoni na utoro uliokithiri.

Sabina Kilenga, mkazi wa kijiji hicho amesema “Baadhi ya wanafunzi walilazimika kuomba usafiri barabarani ili kuwahi masomo, jambo lililoweka watoto wa kike katika mazingira hatarishi na kusababisha mimba za utotoni”. 

Alieleza kuwa hali hiyo ilikuwa chanzo kikubwa cha wanafunzi wengi kushindwa kuhitimu elimu ya sekondari.

Sabina amesema wazazi walilazimika kuwasindikiza watoto wao alfajiri na wakati mwingine kuwasubiri hadi usiku kutokana na umbali wa shule na hofu ya usalama wao.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amesema serikali imeendelea imewekeza katika sekta ya elimu kwa kujenga zaidi ya shule 1,300 za sekondari nchini ili kuhakikisha watoto wanapata elimu karibu na makazi yao.

“Uwekezaji huo unalenga kuongeza usawa wa elimu na kusaidia maendeleo ya taifa kwa kuandaa vijana wenye maarifa na uwezo wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji,” amesema.

1
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kutokana na umuhimu wa shule hiyo serikali inapanga kuanzisha mkondo wa elimu ya ufundi na amali ili wanafunzi wahitimu wakiwa na ujuzi wa vitendo.

Amesema, "Kila siku watu wanajenga nyumba na kununua magari, hivyo vijana wetu wakihitimu kidato cha nne wakiwa na vyeti vya ufundi wataweza kusaidia jamii na kujiajiri badala ya kutegemea ajira chache."

Akisoma taarifa ya mradi, Mhandisi wa Halmashauri Arnold Matambiko amesema serikali ilitoa zaidi ya Sh. milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Amesema fedha hizi zilizotumika kujenga vyumba vinane vya madarasa, maabara tatu, jengo la utawala, jengo la TEHAMA pamoja na matundu 10 ya vyoo.

Matambiko amesema hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha elimu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.