Chalamila azima mgomo w’biashara Simu 2000

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:03 AM Jul 09 2024
Wafanyabiashara wa kituo cha daladala cha Simu 2000 Ubungo jijini Dar es Salaam wakigoma kuhamishwa kutoka katika eneo lao la biashara kwa kile kilichodaiwa kupisha ujenzi wa karakana ya mabasi ya Mwendokasi jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wafanyabiashara wa kituo cha daladala cha Simu 2000 Ubungo jijini Dar es Salaam wakigoma kuhamishwa kutoka katika eneo lao la biashara kwa kile kilichodaiwa kupisha ujenzi wa karakana ya mabasi ya Mwendokasi jana.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara wadogo maarufu machinga katika soko la Simu 2000 kusitisha mgomo na kuendelea na majukumu yao huku akiwaahidi kuzungumza nao Julai 13, mwaka huu, kuwapa msimamo wa serikali.

Jana wafanyabiashara hao waligoma na kuziba barabara kuzuia magari kuingia katika kituo cha mabasi wakilalamikia uamuzi wa kukabidhi eneo hilo kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ili kujenga karakana.

Akizungumza na wafanyabiashara hao jana, Chalamila alikiri suala hilo lipo, lakini halijafikishwa ofisini kwake ili atoe uamuzi kwa kuwa alimwagiza Mkuu wa wilaya hiyo, Hassan Bomboko, walijadili kwanza kwenye mikutano ya wilaya kisha wampelekee.

Aliwaomba wampe muda ili azungumze na DART, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Manispaa ya Ubungo na kuja kuzungumza nao ili wawaeleze msimamo wao.
 Alisema suala hilo linahitaji umakini katika kulitafutia ufumbuzi kwa kuwa wafanyabiashara hao wamehangaishwa kwa kuhamishwa maeneo.

"Jambo la kwanza siku nyingine mimi kaka yenu nipo, jambo lolote likitokea Ofisi ya RC (Mkuu wa Mkoa) ipo wazi, kabla hamjachukua uamuzi wowote jiridhisheni pia RC analijua hili? Pamoja na kwamba shughuli zimesimama nitakapoondoka hapa endeleeni na shughuli zilizopo,” aliagiza.

Awali, Mkuu wa wilaya Bomboko alifika kwa ajili ya kuzungumza na wafanyabiashara hao, lakini walikataa kuzungumza naye na kumtaka aondoke kwa madai kuwa hawana imani naye.

Machinga hao walisema wamelalamikia mara kwa mara kuhusu changamoto zinazowakabili katika eneo hilo na kuwaahidi kwenda kuzifanyia kazi, lakini hakufanya hivyo.


 DC ASHANGAZWA

Akizungumza na waandishi wa habari, Bomboko alisema anashangazwa na uamuzi waliochukua wafanyabiashara hao kwa kuwa hakuna taarifa zozote kuwa eneo hilo limekabidhiwa kwa DART.

Aidha, alisema walikuja hapo kujiridhisha kama kweli wafanyabiashara hao wamesitisha shughuli zao kutokana na madai hayo na kutaka kufahamu kutoka kwao kuwa taarifa hizo zimetangazwa na kiongozi gani wa serikali.

“Manispaa ya Ubungo ndio iliwajengea wafanyabiashara hao vibanda na ndio wamiliki wa eneo hilo, kwa maana hiyo kama kulikuwa na mabadiliko ya matumizi viongozi wa manispaa ndio walitakiwa kutoa taarifa kwa wafanyabiashara,” alisema.

“Lakini hoja ya kwamba soko hili limeuzwa kwa Wachina ni taarifa ambayo na mimi ninaisikia kutoka kwenu, ndio maana nilitaka kujua kutoka kwa wafanyabiashara ni Mchina gani aliyenunua hili soko, lakini pia hizi taarifa zimetangazwa na kiongozi gani wa serikali,” alihoji.

Alisema kilichofanyika katika eneo hilo ni vita za kisiasa ili serikali iache kufanya masuala ya msingi na  kuacha mambo yaende kiholela, aliwasihi wafanyabiashara waendelee na biashara zao na wenye malalamiko waende ofisini wakazungumze.
 Mmoja wa wafanyabiashara hao, Iddi Ramadhani alisema, hawakubaliani na uamuzi wa kuwaondoa wafanyabiashara 2000 na kuweka kituo cha DART chenye magari takribani 230, jambo ambalo si la kiungwana.

“Sisi ni wafanyabiashara tuliotoka barabarani na kuja kukaa sokoni kwa kuheshimu kauli ya Rais Samia, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, alituthibitishia kuwa hili ni soko na tukae kwa amani, leo mtu anakuja anakwambia kuwa wamebadilisha matumizi anatakiwa apewe DART, kwamba DART anathamani kuliko sisi tuliowekeza kwa miaka sita,” alihoji.