CHADEMA yakana kauli yenye utata ya BAZECHA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:07 AM Oct 03 2024
Mwenyekiti wa BAVECHA, Hashim Juma.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa BAVECHA, Hashim Juma.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepinga kauli iliyotolewa na Baraza la Wazee wa chama hicho (BAZECHA) zenye viashiria vya udini na ukabila kikisema sio msimamo wao.

Juzi Mwenyekiti wa BAVECHA, Hashim Juma akizungumza katika hafla ya kusherehekea Siku ya Wazee Duniani alitoa kauli zinazoashiria udini na ukabila ikiwamo kumshangaa Rais Samia Suluhu Hassan kutosalimia kama dini inavyomtaka na badala yake anasalimia ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’.

Aidha, alisema aliwasikia mashekhe wakilalamika kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, ana Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu kuwa anamchukia Rais Samia Suluhu kwa sababu ya dini na eneo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, chama hicho hakihusiki na kauli zozote za kibaguzi zilizotolewa.

Alisema taarifa zilizotolewa zenye viashiria vya udini sio msimamo wa chama hicho na zinapaswa kupingwa na kila Mtanzania bila kujali dini, kabila, au mahali alipotoka.

Taarifa hiyo ilieleza pia mamlaka za chama hicho inafuatilia kiini cha kauli hizo na kuchukua hatua kwa mujibu wa Katiba, kanuni na miongozo ya chama.