CHADEMA yahamia katika maombezi kuing'oa CCM

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:47 AM Sep 06 2024
Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.
Picha: Mtandao
Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimegeukia katika maombi, kikiwataka Watanzania kumwomba Mungu ili katika uchaguzi ujao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) king'oke madarakani.

Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Majengo Shimoni, wilayani Muheza, mkoani Tanga.

Alisema wananchi wanapaswa kufanya hivyo kwa kile alichodai CCM inawapa shida wananchi katika nchi yenye utajiri.

Mnyika alisema Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa, lakini wanaofaidika ni viongozi huku wananchi wakibaki maskini.

Katibu Mkuu huyo pia alionya watendaji wa serikali kuacha mara moja tabia aliyodai "kuibeba CCM katika uchaguzi", akisisitiza CHADEMA wako macho kuhusu hilo.

Katika hilo la madai ya watendaji wa serikali kuibeba CCM, akiwa mkoani Arusha jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisisitiza chama hicho kinashinda kwa haki na kitaendelea kushinda kwa haki kutokana na mikakati yake, ukiwamo utekelezaji ilani ya uchaguzi.

Katibu Mkuu Mnyika pia aliwataja viongozi na wanachama wa CHADEMA kujipanga ipasavyo kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuongoza vijiji, vitongoji na mitaa nchini. 

"Viongozi wa CHADEMA na wanachama mnapaswa kujiandaa ili kushiriki na kushinda nafasi za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa ili kuibwaga CCM," alisema.

Mnyika alisema ushindi wa nafasi hizo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakuwa mwanga na dira ya ushindi wa Uchaguzi Mkuu mwakani katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani.

Aliwataka wananchi kuacha kile alichokiita "uteja wa CCM" badala yake wakikatae kuanzia uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa kuichagua CHADEMA.

Alisema serikali imeleta ugumu wa maisha kwa kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi hasa kwa bidhaa muhimu ikiwamo sukari.

Mbunge mstaafu wa Viti Maalum CHADEMA, mkoani Tanga, Yosepha Komba, alidai kuna baadhi ya viongozi wa CCM wanatuma vijana wao kuharibu bendera za CHADEMA nyakati za usiku.