KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amewataka wana CCM kutowapuuza wapinzani wanaohamia kwenye chama hicho. Badala yake amewataka wawatumie kupata mikakati iliyokuwapo kuelekea uchaguzi.
Akizungumza na wananchi katika Kata ya Engusero, Kiteto mkoani Manyara, alisema katika ziara yake kwenye mikoa ya Arusha na Manyara, idadi ya wanachama wa upinzani na viongozi wao wanaohamia CCM ni kubwa na inazidi kuongezeka.
"Tufanye nao kazi watatusaidia. Kama Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) wilaya anaondoka aliacha mikakati ya chama huko (kwenye vyama), maana yake atakisaidia chama kushinda uchaguzi, hivyo tuwatumie wanachama na viongozi wao ili tupate siri za upande mwingine (upinzani)," alisema Makalla.
Pia alisema umaarufu wa vyama vya upinzani umepungua kutokana na kuwa vya matukio pekee, huku wanachama wao wakikimbilia CCM hali inayoonesha ndicho chama cha matumaini.
Kwa mujibu wa Makalla, CCM ni chama kinachoaminika na chenye wajibu wa maisha ya Watanzania, hivyo kitaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Aidha, Makalla aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Wakazi la Kijiji kuanzia Oktoba 11 hadi 20, mwaka huu, ili wapate sifa ya kuchagua Novemba 27, mwaka huu, na kuwa na uhakika wa ushindi wa CCM.
"Ninawaomba tutumie nafasi hiyo tujiandikishe ili kuipa CCM ushindi. Ninafurahi katika vijiji 66 na mitaa 20 tunataka yote iende CCM," alisema.
Pia alisema CCM haitaki watu kuteuana kwa kujuana au urafiki bali anayekubalika na kuaminiwa na wananchi, na kwamba chama hicho hakipo tayari kupewa mgombea wa kumsafisha kwa dodoki.
"Zipo sababu nyingi za kuwaomba mtuchague, tumetekeleza Ilani ya uchaguzi, nilivyofika Kiteto leo sio ya miaka 1998, kuna mtu anaweza kusema Kiteto haina maendeleo, akikwambia hivyo jua ana matatizo ya akili au ni mgeni," alisema.
Kwa mujibu wa Makalla, CCM inawajibu na dhamana ya kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kukiamini na kuendelea kukiweka madarakani.
Alisema Barabara ya Kiteto hadi Njiapanda NARCO serikali imaishughulikia ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Pia alilaani matukio la ulawiti baada ya tukio la mama na mwanawe kulawitiwa na kuuawa, na kuwataka viongozi wa dini kukemea.
Aidha, aliwataka wananchi kutowaamini waganga kwa kuwa ni waongo na kusababisha matatizo kwenye jamii kwa kucheza na akili za watu.
"Imani za kishirikina zisitupelekee kutenda maovu, Jumuiya ya Wazazi, Jumuiya ya Wanawake kemeeni na kuendelea na kampeni ya kupiga vita matukio haya," alisema.
Kiongozi huyo alipokea kero 85 za elimu, wajasiriamali kudhulumiwa Sh. milioni 100, eneo la malisho kubadilishwa matumizi, wanyamapori, uchaguzi wa mbunge na diwani urudishwe kwa wanachama wote, shule yenye walimu wa kiume pekee, ubovu wa barabara vijijini.
Zingine ni kukosekana kwa maneneo ya malisho, malumbano kati ya wakulima na wafugaji, ahadi ya mifuko 100 ya aliyekuwa Katibu Mkuu katika Zahanati ya Chapakazi na nyumba ya watumishi.
Kero zingine ni migogoro ya mipaka, kikundi cha VICOBA kudhulumiwa na viongozi wa kikundi kukimbia na jengo lao kuchukuliwa, upatikanaji mdogo wa maji, kutolipwa fedha za mbaazi, ombi la barabara kuwekwa lami, kuporwa eneo la kijiji.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Redimas Mwema, alisema waliokutwa wanalima ndani ya nyanda za malisho lakini mgawo haukuwatambua, na kwamba kamishna wa ardhi atafika kutambua waliokutwa kwenye nyanda hizo na kuwatambua wavamizi ambao wameshajulishwa wanatakiwa kuondolewa.
Alisema kuna viongozi wa vitongoji na vijiji kualika wageni kutoka nje ya wilaya ambao wanamiliki maeneo makubwa kwani kuna wenye ekari 400 hadi 500 na kwamba wamewapata wawili na wamewaambia waache ila wanaendelea na kwamba kwa sasa wanataka kuwapeleka mahakamani.
Awali, Mwema alisema kuna changamoto na taswira kwamba wilaya ya Kiteto ina migogoro mingi na kwamba walikuja na kaulimbiu ya "Wilaya ya Kiteto Migogoro Haina Nafasi Maendeleo Ni Kipaumbele."
Pia alisema alisema migogoro mingi ya ardhi ndani ya wilaya inasimamiwa kikamilifu na kushughulikiwa kikamilifu na kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani jumla ya tani 1,867 zimeingia kwenye mnada na wanauza mbaazi kwa bei wezeshi kwao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED