ALIYEKUWA Meya wa Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam Boniface Jacob maarufu kama 'Boni Yai' amepata dhamana, baada ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri kupinga dhamana ya kada huyo.
Jacob amepata dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wenye barua za Serikali za Mitaa na kusaini bondi ya sh milioni saba na pia ametakiwa asitoke nje ya nchi bila kibali cha Mahakama.
Uamuzi huo mdogo, umetolewa leo Oktoba 7,2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga alisema kuwa kiapo cha RCO wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Davis Msangi hayana maelezo yaziada ya kutosha kuzuia dhamana hiyo ya Jacob.
Alisema sababu zilizotolewa hazina maelezo ya ziada ya kwanini mahakama isitoe dhamana, kwamba iwapo mjibu maombi ametoa maelezo juu ya usalama wake alitegemea muombaji (Jamhuri) kupeleka uthibitisho juu ya maelezo ya mjibu maombi (Jacob).
"Upande wa majibu maombi haujaleta kiapo kinzani lakini kiapo cha muombaji haitoshi Mahakama kumnyima dhamana mtuhumiwa ukizingatia hii ni haki yake ya Kikatiba,"alisema Hakimu Kiswaga
Kutoka na hali hiyo, Makama ilikubaliana maombi ya Jamhuri hivyo basi mjibu maombi atapewa dhamana kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na mahakama hiyo, ambayo mshtakiwa ameyatimiza.
Kada huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jacob anatuhumiwa kwa mashtaka mawili likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wake wa kijamii.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ilidaiwa kuwa Septemba 12, 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam alichapisha taarifa kwenye mtandao wa X zamani Twitter wenye jina la Jacob ex Meya Ubungo uliyosema"Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji ya moja kwa moja katika kuwapoteza watu wa baadhi ya familia zoa,Kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba,kupotea kwa Deo Mugasa,kupotea kwa Adnandi Hussein Mbezi na kupotea kwa vijana watano wa Aggrey kupitia akaunti hiyo kwa lengo la kuleta taharuki kwa jamii.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED