Biteko: Uzalishaji umeme haukidhi mahitaji

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 01:39 PM Apr 25 2024
Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

SERIKALI imesema licha ya ongezeko la uzalishaji umeme kwa asilimia 14.2 katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, mwaka huu, bado kiwango hicho hakikidhi mahitaji ya taifa, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema hayo bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/25.

Katika makadirio hayo, Dk. Biteko ameliomba bunge kuidhinisha  Sh. trilioni 1.883 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za wizara hiyo.

Biteko ametaja sababu zingine za upungufu wa umeme kuwa ni pamoja na upungufu wa maji na gesi asilia katika vituo vya kufua umeme, hitilafu katika mitambo ya uzalishaji na kufanyika kwa matengenezo katika mitambo ya uzalishaji wa nishati hiyo. 

Amesema mahitaji ya juu ya umeme nchini yamekuwa na kufikia megawati 1,590.1 zilizofikiwa Machi 26, mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ikilinganishwa na megawati 1,470.5 zilizofikiwa Juni 12, 2023.

MAFANIKIO

Dk. Biteko amesema hadi Machi, mwaka huu, hali ya uzalishaji wa umeme imepanda kwa asilimia 14.2 ikiongezeka kutoka megawati 1,872.1 hadi megawati 2,138 kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme unaoendelea nchini kutoka umeme uliounganishwa katika gridi ya taifa.

Amesema  katika kiasi hicho, megawati 836.3 sawa na asilimia 39.1 ni umeme unaotokana na nguvu ya maji, megawati 1,198.8 sawa na asilimia 56.1 unatokana na gesi asilia, megawati 92.4 (asilimia 4.3) mafuta mazito na magawati 10.5 (asilimia 0.5) ni kutokana na tungamotaka (biomass).

“Ongezeko la uwezo wa uzalishaji wa umeme limetokana na kuanza kwa uzalishaji wa umeme kupitia Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115. tayari  uzalishaji umeanza kwa megawati 235 kupitia mtambo mamba tisa. Matarajio  ni mradi huu kukamilika Desemba, 2024 kwa mitambo yote minane yenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kila moja kuwa inazalisha umeme.

”Vilevile kukamilika kwa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rusumo ambao unachangia megawati 26.7 katika gridi ya taifa, kukamilisha ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I Extension megawati 185. kwa  sasa mitambo yote minne  inafua umeme kiasi cha megawati 40 kila mmoja, hivyo kuwezesha uzalishaji wa umeme kuingizwa katika gridi ya taifa,” amesema.

Pia ametaja ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa jua mkoani Shinyanga wa megawati 150 unaendelea na kuwa matarajio ni umeme huo kuanza kuzalishwa ifikapo Januari, 2025.

Aidha, amesema hadi kufikia Machi 2024, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme ambayo haijaungwa katika gridi ya taifa ni megawati 33.4 ambazo zinajumuisha mitambo inayomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO0 yenye uwezo wa kufua megawati 28.4 na megawati tano zitokanazo na nguvu ya jua kutoka kwa mzalishaji binafsi.

Biteko amesema wizara kupitia TANESCO inanunua umeme wa megawati 31 kati ya hizo  21 kutoka Uganda kwa ajili ya mkoa wa Kagera na zingine 10 kutoka Zambia kwa ajili ya mkoa wa Rukwa.

Amesema serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na Malagarasi (megawati 49.50, Ruhudji (megawati 358), Rumakali (megawati 222) Kakono (megawati 87.8) na Kikonge megawati 321 na utekelezaji wake umefikia katika hatua mbalimbali.