Bil 1.56/- kuendeleza kilimo ikolojia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:09 PM Feb 21 2026
news
Picha Mpigapicha Wetu
Bil 1.56/- kuendeleza kilimo ikolojia

VITUO sita vya kilimo ikolojia hai nchini, vinavyotekeleza Mradi wa AgroKilimo, vimekutana katika warsha ya siku tatu kwa ajili ya kuchanganua na kujadiliana namna ya kuendeleza kilimo hicho kwa wakulima.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shiriki la Islands of Peace (IDP), Ayesiga Buberwa wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa warsha hiyo ya siku tatu iliyofanyika kwenye Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Hai (SJS) Kwanyange wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Buberwa amesema Mradi wa AgroKilimo unafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa kwa Euro laki 515 (sawa na Sh. Bilioni 1.56) kwa miaka miwili, umechagua vituo sita vya majaribio ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kujenga mustakabali imara na endelevu wa kilimo hicho 

"Mpango huu unalenga kuimarisha vituo vya majaribio kote nchini. Kwa msaada wa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, mradi huu unalenga kujenga ujuzi, kusambaza maarifa, na kuunda mtandao thabiti wa kitaifa wa vituo vinavyokuza ubunifu katika kilimo ikolojia," amesema.

Pia mradi huu utafadhili utafiti wa Shahada ya Uzamili kwa wanafunzi wanaosoma Kilimo ikolojia na kushirikiana kwa karibu na Kitovu cha Kilimo Ikolojia Tanzania (AEHT), ambacho ni kitovu kikuu cha utafiti wa mradi, kikiunganisha washirika wote wa kilimo hicho katika masuala ya utafiti.

Amesema katika warsha hiyo, kila kituo kilipitia vipengele muhimu vya kazi zake, ikiwemo historia yake, muundo wa shirika, mbinu za utafiti na mafunzo, miundombinu na vifaa, usimamizi wa wafanyakazi, bajeti na mifumo ya ufadhili, ulinganifu na mfumo wa Wizara ya Kilimo, pamoja na mipango ya muda mrefu ya uendelevu.

Amesema Mradi wa Agro Kilimo ulizinduliwa mwaka 2025 na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne-Sophie Avé ambapo mradi umejengwa katika nguzo kuu mbili. 

Amesema nguzo ya kwanza ni kufanya na kuthibitisha tathmini shirikishi ya namna vituo vya kilimo ikolojia vinavyoendeshwa nchini Tanzania. 

"Nguzo ya pili ni kuandaa njia za vitendo za kuviwezesha vituo kuunganishwa katika mtandao pamoja na kuunda miongozo ya pamoja ya utafiti, maendeleo, na mafunzo. 

Hii inajumuisha utafiti wa matumizi na utafiti wa ulinganishaji wa mazao katika mazingira tofauti, kuwashirikisha wakulima katika shughuli za utafiti, mbinu shirikishi za ugani, na mifumo endelevu ya mafunzo ya kitaaluma.

Akizungumzia warsha hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa PPIZ, Ikram Ramadhan Soraga amesema mradi huo umekuja wakati muafaka na utaenda kuleta mabadiliko ya kilimo ikolojia hai Zanzibar.

Naye Felician Pius wa SJS, amesema ujio wa mradi wa AgroKilimo ni muhimu kwao kwani dhamira yao ni kuirejesha sekta ya kilimo kwenye mfumo wake wa zamani ambao ni salama.

Meneja Msaidizi wa MFEC, Peter Mwita amesema mradi huo unaenda kuendeleza mapambano yao kwenye eneo la kilimo ikolojia, ikiwemo kuboresha miundombinu ikiwemo uvunaji wa maji na mengine.