BAKWATA yataka Tume Huru kuchunguza utekaji na mauaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:34 AM Sep 17 2024
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakary Zubeir  Bin Ally, katika Baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu, Geita, jana.
PICHA: OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakary Zubeir Bin Ally, katika Baraza la Maulid Kitaifa lililofanyika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu, Geita, jana.

BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limeshauri serikali kuunda tume huru kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa matukio ya watu kutekwa na kuuawa yanayoripotiwa nchini.

Kukiwa na rai hiyo ya BAKWATA, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa amesema serikali inafanyia kazi changamoto hiyo ya kiusalama, akidokeza kuwa "kuna baadhi wameanza kuleta chokochoko katika taifa". 

Rai ya kuundwa tume huru ya uchunguzi wa matukio ya utekaji na mauaji nchini ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Alhaj Nuhu Mruma, wakati wa maadhimisho ya Baraza la Maulid yaliyofanyika kitaifa mkoani Geita kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu. 

Alisema Baraza hilo linaendelea na litaendelea kupinga matukio ya ukatili na utekaji kwa kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kuthaminiwa utu wake. 

"Tume hiyo itakapoundwa ikatende haki kwa kuzingatia sheria. Kwa kuwa huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwakani Uchaguzi Mkuu, ni vyema ukafanyika kwa uhuru na haki," alisema. 

Alhaj Mruma pia alitoa wito kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura pamoja na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Kiongozi huyo wa BAKWATA pia alitoa wito kwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi kutenda haki na kufuata taratibu zote za uchaguzi. 

“Vyama vya siasa pia epukeni rushwa kwani itasababisha kutokuwapo kwa haki," Alhaji Mruma alitoa angalizo. 

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dk. Abubakar Zuber bin Ally, aliwataka Watanzania na waamini wa dini hiyo kulinda amani ya nchi na kuwa na maadili mema. 

Mufti Zubeir aliwataka pia Waislamu na Watanzania kushikiri katika ujenzi wa uchumi wa nchi, ukiwamo ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta za elimu na afya, akisema, "Waislam tujenge na tulinde uchumi wetu, tusomeshe watoto ndani na nje ya nchi." 

Vilevile, Mufti alitoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo na kulinda nchi yao, akisisitiza kuwa “kufanya hivyo ni wajibu wa kila mmoja, tuichunge na tuipende nchi yetu, ni muhimu kwa kila Mtanzania kushiriki katika kuzuia mmomonyoko wa maadili." 

Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Baraza hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa wakati huu ni muhimu kwa nchi kushikamana na kuwa wamoja katika kulinda amani ya nchi kuelekea uchaguzi. 

Kuhusu matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea nchini, Majaliwa alisema serikali inaendelea kukabiliana nayo na kuwa tayari Rais Samia alikwishaunda Tume ya Haki Jinai inayoshughulikia masuala yanayoendana na hayo, hivyo kuwataka Watanzania kuendelea kuwa na imani na serikali yao. 

"Kuna baadhi wameanza kuleta chokochoko katika taifa hili, lakini hatua kali zitachukuliwa. Suala muhimu ni kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake na pale linapotokea suala linalotiliwa shaka, litolewe taarifa mapema iwezekanavyo," aliagiza Majaliwa. 

Waziri Mkuu alitoa wito kwa viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla wahakikishe wanasimamia na kuimarisha maadili mema kwa jamii ili kuepuka maovu na kuleta maendeleo endelevu nchini. 

"Nitumie fursa hii kuendelea kutoa rai kwa wananchi, wazazi na viongozi wa dini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wetu katika ngazi zote kwa kuzingatia maadili na tamaduni ya taifa letu. Ni wajibu wetu kama wananchi," alisema. 

Majaliwa alisema kuwa viongozi wa dini wana jukumu la kutoa mwongozo na malezi ya kiroho kwa waumini kwa kuwa wana nguvu kubwa ya kuhamasisha maadili na tabia nzuri. 

"Wazazi, ninyi mna jukumu la msingi katika kulea watoto wenu kuanzia katika ngazi ya familia ili kujenga tabia njema, na tukifanya hivyo matendo ya ovyo hayatakuwapo, lazima tuwe macho katika matendo haya ambayo yanaweza kuleta hofu kwa jamii yetu," alisema. 

Majaliwa alisema kuwa kila mmoja anapaswa ashiriki katika kulinda taifa kwa kutambua matendo yote yanayoashiria uvunjifu wa amani ili nchi iendelee kuwa imara. 

"Suala la ulinzi na usalama ni letu sote Watanzania, ndivyo tulivyofanya tangu Tanzania ipate uhuru," Waziri Mkuu alisema. 

Aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kutumia sherehe za Maulid kwa kuonesha kwa vitendo namna ya kuishi kwa upendo, heshima, maadili, huruma na uadilifu. 

"Kwa kuenzi maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W), tutumie sherehe za Maulid kuwa chanzo cha mabadiliko chanya katika maisha ya waumini. Sote tutumie nafasi hii kuhamasika na kujitahidi kuishi kwa maadili ya Mtume, ambayo yanajumuisha tabia nzuri, uadilifu na huruma," alisema. 

Rai ya BAKWATA kuhusu kuundwa tume huru ya kuchunguza matukio ya utekaji na mauaji nchini, imetolewa siku moja baada ya 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuunga mkono hoja ya kuchunguza matukio hayo. 

Ikiwakutanisha viongozi wandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Dar es Salaam juzi, TEC ilionya kuwa tunu za undugu na amani nchini zimeshambuliwa kutokana na matukio ya kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa Watanzania yanayoendelea.  

Viongozi hao ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi.  

Akiwatambulisha viongozi hao juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, alisema walikwenda kushiriki Kilele cha Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu la Kitaifa.  

Padri Kitima aliwaita na kuwasimamisha kwa pamoja viongozi hao jukwaani kuwatambulisha kisha aliwakumbusha kuwa wao ni ndugu, hivyo wakaishi kwa upendo, wakapeleke tunu ya injili na kusambaza upendo katika vyama vya siasa. 

Alisema historia ya viongozi inaonesha kuwa walilelewa kwenye misingi ya kikatoliki, hivyo wakaienzi Ekaristi kwa kuendeleza upendo na undugu.  

Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Eusebius Nzigilwa, alisema kuwa hivi sasa tunu za undugu na amani ya nchi zimeshambuliwa kutokana na matukio ya kuteka, kutekwa, kuumizwa na kuuawa Watanzania.

 Alisema Tanzania kwa miaka mingi inajulikana kama kisiwa cha amani, udugu na mahali pekee Afrika ambapo raia wake wameendelea kuishi kwa umoja, amani na undugu licha ya tofauti zao za kikabila, kiimani, kiitikadi na kiuchumi.  

"Tunajiuliza nini kimepotea kwenye tunu yetu hii? Taifa letu limepotea wapi? Je, uongozi na mamlaka husika pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimezidiwa nguvu na maarifa hata kushindwa kudhibiti hali hii?” alihoji.  

Alisema TEC haiamini kama makundi hayo ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vya ulinzi na usalama na kuviomba vitimize majukumu yao, ili kurudisha heshima ya taifa ya kuwa kisima cha undugu na amani. 

 "Tunaunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na haraka, ili wale wote waliohusika na matukio hayo yafikishwe mbele ya sheria," alisema.