Asasi za kirai zatakiwa kutafuta njia mbadala kujiendesha

By Allan Isack , Nipashe
Published at 01:01 PM Sep 16 2024
Mwenyekiti wa Bodi ya AZAKI ,Mercy Silla, akizungumza wakati wa kufunga Wiki ya AZAKI.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya AZAKI ,Mercy Silla, akizungumza wakati wa kufunga Wiki ya AZAKI.

ASASI za kiraia nchini zimetakiwa kutafuta njia mbadala ambazo zitawasaidia kujitegemea kuendesha shughuli zao katika kijamii pamoja na kutoa elimu ya kutosha ili kuchochea na kuboresha maendeleo kwa wananchi.

Hayo yalisemwa   na Mwenyekiti wa Bodi ya AZAKI, Mercy Silla, wakati akifunga Wiki ya AZAKI iliyofanyika kwa  mkoani Arusha kwa siku tano.

Silla, alisema kuwa, kukutanisha asasi hizo wiki nzima wameweza kujadili maswala mbalimbali ya kuboresha katika utendaji kazi sambamba na kujifunza zaidi kutoka kwa wenzao wa nje ya nchi.

Alisema ni wajibu wao kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele ili kuongeza ushiriki wa kutosha katika shughuli mbalimbali za kijamii na kuhakikisha jamii unanufaika nazo kwa kiwango kikubwa. 

“Ni wakati wetu  kuhakikisha sasa vijana wetu wananufaika na fursa mbalimbali za kibiashara na kuhakikisha tunajenga uelewa wa kutosha kwa jamii na kamwe tusiache kuchochea uboreshaji ili kuboresha bunifu kwenye mchakato wa kijamii.”alisema Silla.

Licha ya kuzungumza hayo,alisema mkutano huo wa wiki nzima umeweza kuongeza uelewa wa hali ya juu kwa vijana na kuweza kuzitambua haki zao ikiwa ni pamoja na kupata elimu ya kuweza kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo nchini.

Mratibu wa mabadiliko ya tabia nchi kutoka  shirika la ActionAid, Happy Itroz, alisema kuwa, kuna  haja ya elimu kutolewa  zaidi kuhusu maswala ya kilimo ikolojia kwani bado kilimo.hicho hakijapewa kipaumbele kwa wakulima kwani kuna mafanikio makubwa sana endapo wakulima watakitumia  .

Hata hivyo alizitaka benki kuhakikisha wanatoa  mkopo wa riba nafuu kwa wakulima ili  waweze kunufaika na mkopo na kuweza  kuboresha kilimo chao na kuondokana na kilimo cha mazoea na kulima kilimo chenye  tija  na kuweza kuongeza kipato zaidi.