Aliyemuua mkewe kwa kunyimwa tendo la ndoa ashindwa rufani

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 11:02 AM Sep 16 2024
Mahakama ya Rufani Tanzania.
Picha: Mtandao
Mahakama ya Rufani Tanzania.

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imetupilia mbali rufani iliwasilishwa na Erick Buberwa aliyefungwa miaka minane kwa kumuua bila kukusudia mkewe kwa kumnyima tendo la ndoa kwa sababu haina mashiko.

Hukumu hiyo ya mahakama ilitolewa juzi Mahakama ya Rufani Dar es Salaam mbele ya jopo la majaji watatu; Jaji Ferdinand Wambali, Jaji Lilian Mashaka na Jaji Benhaji Masoud baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.

Mrufani Buberwa aliwasilisha rufani dhidi ya Jamhuri, akipinga adhabu ya kifungo cha miaka minane alichohukumiwa na Mahakama Kuu kwa kumuua bila kukusaidia mkewe Mercy Mukandala Juni, 2020.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Juni 16, 2020, huko Kimara, majira ya usiku, mrufani na mkewe, wakiwa chumbani wamelala, mrufani aliomba kupewa haki yake ya ndoa lakini mkewe alikataa kumpa. 

Inadaiwa katika kutofautiana huko, alimwambia mkewe ana mwanamume mwingine anayempenda kuliko yeye kisha akainuka kuelekea jikoni na kurudi na spana ya kufungulia bomba akiwa na lengo la kumpiga nayo mrufani, badala yake mrufani alimpigia nayo mkewe kichwani.

Mkewe aliangukia meza huku akiwa na jeraha, alivuja damu, mrufani aliwafahamisha majirani; walimchukua kumpeleka hospitali lakini alifariki dunia akiwa njiani. 

Inadaiwa mrufani aliripoti polisi na mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Pwani (Tumbi) kwa ajili ya uchunguzi ambako kifo chake kilibainika kusababishwa na majeraha kichwani yaliyosababisha kuvuja damu na kupoteza maisha.

Mrufani alifikishwa mahakamani kwa mashtaka ya mauaji ya bila kukusudia na baada ya usikilizwaji, alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka minane gerezani kwa kuua bila kukusudia.

Baada ya adhabu hiyo, mrufani aliwasilisha rufani mahakamani akipinga adhabu akiwa na sababu mbili; kwanza ni kwamba mahakama haikuzingatia kwamba ni mkosaji wa mara ya kwanza na haikuzingatia maombolezo yake ya kupunguziwa adhabu.

Sababu ya pili anadai mahakama haikuzingatia kwamba kifo kilitokana na kunyimwa haki yake ya ndoa na maneno yaliyotamkwa na marehemu kuwa ana mwanamume mwingine anayempenda zaidi yake.

Mrufani katika usikilizwaji aliwakilishwa na Wakili Musa Mhagama huku wajibu rufani wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Job Mrema, akisaidiana na Wakili wa Serikali John Mwakifuna.

Wakili Mhagama aliomba kuondoa sababu ya pili na kubakia na sababu ya kwanza kwamba mazingira ya utendaji kosa hayakuzingatiwa na mahakama haikuzingatia kuwa mrufani amebaki na jukumu la kulea mtoto wao mdogo.

Alijibu hoja za rufani, Wakili Mrema alidai mahakama ilitenda haki kisheria, ilizingatia mazingira yote ya utendaji kosa na kwamba aliomba Mahakama ya Rufani imwongezee adhabu mrufani kutoka miaka minane jela hadi miaka 20 jela.

Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, jopo lilisema kwamba kabla ya kuhitimisha, wanaona inafaa kutoa maoni yao kwa mwaliko uliotolewa na Wakili Mrema kwamba mahakama iitishe maombi yake kwa mamlaka iliyonayo kisheria kuongeza kifungo cha miaka 10 impe mrufani kifungo cha miaka ishirini jela. 

"Sisi kwa heshima tunakataa mwaliko wa Wakili Mrema, kwa maoni yetu Jamhuri ambaye ni mlalamikiwa ilipaswa kuwasilisha rufani mtambuka kama alikuwa hakuridhishwa na adhabu.

"Hakuna rufani nyingine mbele yetu. Hivyo, hatuoni sababu ya kuingilia kati hukumu ya Mahakama Kuu. Kwa kusema hayo, mwombaji anapaswa kutumikia kifungo cha miaka minane kilichotolewa na Mahakama Kuu," lilisema jopo.

Mahakama ya Rufani iliona rufani haina mashiko, hivyo ikatupiliwa mbali.